Dar es Salaam — Tukio la kila mwaka la kuwawezesha wanawake kiuchumi, Women Shaping the Future (WSF) 2026, linatarajiwa kufanyika Jumamosi, Machi 28, 2026 katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, likiwa na lengo la kukuza uelewa wa kifedha na ujenzi wa ukwasi kwa wanawake nchini.
Tukio hilo linaloandaliwa na Studiored Communications (SRC), limebeba kaulimbiu isemayo “Jenga Ukwasi. Jenga Nguvu.”, likilenga kuwajengea wanawake uwezo wa kubadili kipato kuwa mali, kulinda utajiri na kuunda urithi wa kudumu kwa vizazi vijavyo.
Katika toleo la mwaka huu, Stanbic Bank Tanzania imejiunga kama mshirika rasmi wa tukio, hatua inayodhihirisha dhamira ya taasisi hiyo katika kuendeleza uwezeshaji wa kifedha kwa wanawake kupitia elimu, ushauri wa uwekezaji na programu za maendeleo ya ujasiriamali.
Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mkuu wa Kitengo cha Corporate & Investment Banking wa Stanbic, Ester Manase, alisema kuwa uwezeshaji wa wanawake kifedha ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Tunataka kwenda zaidi ya hamasa kwa kutoa mikakati ya kifedha inayotekelezeka itakayowawezesha wanawake kujenga, kukuza na kulinda mali zao kwa ujasiri,” alisema.
Tukio hilo linatarajiwa kukutanisha wanawake viongozi, wataalamu, wajasiriamali na watoa maamuzi zaidi ya 200, likiwa jukwaa la majadiliano ya kina kuhusu uundaji wa ukwasi, uwekezaji na urithishaji wa mali.
Mgeni rasmi katika tukio hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, ambaye atatoa hotuba kuu akisisitiza nafasi ya wanawake katika uchumi wa taifa na dira ya maendeleo ya muda mrefu.
Programu ya WSF 2026 itajumuisha vipindi mbalimbali vya kitaalamu ikiwemo majadiliano ya jopo yenye mada “Utajiri Bila Ruhusa: Jinsi Wanawake Wanavyojenga Nguvu, Umiliki na Urithi,” yatakayowakutanisha wataalamu kama Sophia Byanaku, Tumaini Pyanisa na Wanda Gordon.
Aidha, kutakuwa na darasa maalum la Wealth Studio Masterclass litakaloongozwa na mtaalamu wa fedha Emilian Busara, likilenga kuwapatia washiriki mbinu za vitendo kuhusu ujenzi na usimamizi wa mali.
Akizungumza kwa niaba ya waandaaji, Tanya Mulamula alisema kuwa lengo la tukio hilo ni kuhakikisha wanawake wanapata maarifa ya kina na mikakati inayoweza kutekelezeka.
“Tunataka kila mwanamke anayehudhuria aondoke na mpango mahususi wa kifedha, siyo hamasa pekee,” alisema.
Toleo la mwaka huu linafuatia mafanikio ya WSF 2025 lililowakutanisha zaidi ya washiriki 120 na wazungumzaji 15 kutoka sekta mbalimbali, hatua inayoonesha kuongezeka kwa uhitaji wa majukwaa ya kujenga uwezo wa wanawake kiuchumi.
WSF 2026 inatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha mabadiliko ya kiuchumi kwa wanawake, huku ikiendelea kuhamasisha ujenzi wa jamii yenye usawa na ustawi wa pamoja.



Toa Maoni Yako:
0 comments: