Angalizo! Picha hii ni mfano wa tukio ila si halisi.
Na Mwandishi Wetu, Tabora
Jeshi la Polisi Tanzania limemkamata mkazi wa Kijiji cha Imalamakoye B, Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, kwa tuhuma za kumfanyia ukatili mtoto wa miaka 10 kwa kumfunga kamba mikono na miguu kisha kumnining’iniza dirishani.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu Dodoma Machi 4, 2026, tukio hilo lilitokea Machi 2, 2026 katika Wilaya ya Urambo. Mtuhumiwa aliyetajwa kwa jina la Joseph Mbalamwezi Fransis, ambaye ni mjomba wa mtoto huyo na wanaishi nyumba moja, anadaiwa kutekeleza kitendo hicho kinyume na sheria.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtoto huyo aliokolewa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu mara baada ya tukio hilo kugundulika. Hali yake inaendelea kufuatiliwa huku uchunguzi wa shauri hilo ukiendelea.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni baada ya mtoto kumwaga mboga (nyama) iliyokuwa inapikwa, jambo lililomkasirisha mtuhumiwa na kuamua kumwadhibu kwa njia ya kikatili.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria. Aidha, Polisi wamewashukuru wananchi waliotoa taarifa zilizopelekea kuokolewa kwa mtoto huyo na kukamatwa kwa mtuhumiwa.
Jeshi hilo limekumbusha jamii kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kulinda haki na usalama wa watoto, likisisitiza kuwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto havitavumiliwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika.



Toa Maoni Yako:
0 comments: