
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe chini ya Wizara ya Afya Tanzania, kambi hiyo itahusisha madaktari wabobezi katika fani mbalimbali za tiba ili kusaidia wananchi kupata uchunguzi, ushauri na matibabu ya magonjwa mbalimbali.
Huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na matibabu ya magonjwa ya ndani kama kisukari, magonjwa ya moyo, figo na shinikizo la damu. Aidha, wananchi watapata huduma za kibingwa za macho, sikio, pua na koo pamoja na huduma za upasuaji wa mifupa na upasuaji wa jumla.
Vilevile kutakuwa na huduma za kibingwa kwa watoto, wanawake na uzazi, pamoja na matibabu ya ubingwa bobezi yanayohusu mfumo wa chakula, magonjwa ya moyo na mfumo wa mkojo. Huduma nyingine zitakazopatikana ni pamoja na radiolojia, dawa za usingizi na ganzi salama pamoja na huduma za kinywa na meno.
Akitoa taarifa hiyo kwa umma, Afisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Ombeni S. Utembele, amewahimiza wananchi wenye changamoto za kiafya kufika hospitalini hapo katika tarehe zilizotajwa ili kupata uchunguzi na matibabu stahiki.
Amesema huduma hizo zitatolewa kwa gharama za kawaida za hospitali na pia zitahusisha matumizi ya bima za afya, huku akisisitiza kuwa hospitali hiyo ipo tayari kuwahudumia wananchi wote kwa ubora.
Kambi hiyo inatarajiwa kuwasaidia wananchi wengi wa Mkoa wa Njombe kupata huduma za kibingwa bila kusafiri umbali mrefu kwenda katika hospitali nyingine kubwa nchini.


Toa Maoni Yako:
0 comments: