Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Broadcasting Corporation (TBC), Ayub Rioba Chacha, ameaga rasmi watumishi wa shirika hilo pamoja na Watanzania kwa ujumla baada ya kulitumikia kwa takribani miaka 10 mfululizo.

Akizungumza katika salamu zake za kuaga, Dkt. Rioba alikumbusha kuwa aliteuliwa kushika wadhifa huo tarehe 19 Machi na John Pombe Magufuli, akieleza kuwa kipindi chake cha uongozi kilikumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo presha na upinzani kutoka kwa baadhi ya watu waliotaka aondolewe madarakani.

“Nilipitia vita ngumu sana kutoka kwa wale walioamini nilipaswa kutumbuliwa, lakini nilisimama imara,” alisema.

Dkt. Rioba alimshukuru hayati Dkt. Magufuli kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo ya uongozi, huku pia akitoa shukrani kwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na hata kumteua tena mwaka 2024 kwa kipindi cha miaka miwili ya ziada.

Alisema hatua hiyo ilikuwa ya kipekee kwake, hasa ikizingatiwa mazingira ya uwajibikaji mkali yaliyokuwepo katika vipindi vya uongozi wa marais hao wawili.

“Ninamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, si tu kwa kuninusuru wakati napitia changamoto, bali pia kwa kuniongezea muda wa kuhudumu,” aliongeza.

Katika hotuba yake, Dkt. Rioba aliishukuru menejimenti na wafanyakazi wa TBC kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake, akieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana yalitokana na juhudi za pamoja.

Aidha, aliwataka watumishi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mkurugenzi Mkuu mpya atakayechukua nafasi yake, ili kuendeleza mafanikio ya shirika hilo la umma.

Dkt. Rioba pia aliwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuunga mkono TBC, ama kwa kufuatilia maudhui yake au kushirikiana nayo kibiashara, akisisitiza kuwa uzalendo wao utabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwake.

Alimalizia kwa kueleza kuwa tarehe 19 Machi itaendelea kuwa ya kipekee kwake, kwani ndiyo siku aliyoteuliwa mara ya kwanza, siku aliyoongezewa muda wa uongozi, na pia siku ambayo Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuondoka kwake kunahitimisha ukurasa wa uongozi wa muongo mmoja ndani ya TBC, huku akiacha rekodi ya kuwa mmoja wa viongozi waliodumu kwa muda mrefu zaidi katika nafasi hiyo nchini.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: