Na Mwandishi Wetu

Serikali imeombwa kupunguza gharama za usajili wa vyombo vya habari mtandaoni (online media) ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika sekta ya habari na maudhui ya kidijitali.

Ombi hilo limetolewa Jumamosi, Januari 24, 2026 na Mkurugenzi wa BMG Media, George Binagi, wakati wa hafla fupi ya kupokea tuzo maalum kutoka YouTube baada ya chombo hicho cha habari mtandaoni kufikisha wafuasi (subscribers) laki moja.

Binagi amesema kuwa licha ya Serikali kupunguza gharama za usa jili wa online media kutoka Sh milioni moja hadi Sh laki tano, bado gharama hizo ni kubwa kwa vijana wengi wanaotaka kuanzisha vyombo vyao mtandaoni.

“Tunaomba gharama hizi zipunguzwe hadi Sh laki moja. Hatua hiyo itawasaidia vijana wengi, hususan wahitimu wa vyuo vya uandishi wa habari, kujiajiri na hata kuajiri wenzao,” amesema Binagi.

Ameongeza kuwa kuanzia mwaka huu 2026, watengeneza maudhui mtandaoni wameanza kukatwa asilimia tano (5%) ya mapato yao ya mtandaoni ambayo huwasilishwa serikalini, huku bado wakiendelea kulipa kodi nyingine, jambo ambalo amesema linaongeza mzigo wa kodi na kufanana na kutozwa kodi mara mbili.

Kutokana na hali hiyo, ameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kutatua changamoto hiyo ili kulinda na kukuza sekta ya ubunifu na ajira za kidijitali.

Katika hatua nyingine, Binagi amewashukuru wadau, wasomaji na wafuasi wa BMG Media kwa mchango wao mkubwa uliofanikisha kupatikana kwa tuzo hiyo kutoka YouTube, na kuahidi kuendelea kuzalisha maudhui yenye weledi, ubora na yanayokidhi mahitaji ya jamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa MISATAN na MPC, Edwin Soko, amesema mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali kwa sasa ni fursa muhimu kwa vijana katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Soko amehimiza matumizi sahihi na yenye tija ya mitandao hiyo, akibainisha kuwa inaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira na maendeleo ya kiuchumi endapo itasimamiwa vizuri.

Kuhusu gharama za usajili na kodi mbalimbali, Soko ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesema atayafikisha masuala hayo kwa mamlaka husika kupitia vikao vya wadau wa habari vinavyoendelea kufanyika kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi katika sekta ya habari.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: