Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa CEO Roundtable of Tanzania akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Hoteli ya Hayatt Regency mkoani Dar es salaam, Desemba 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa CEO Roundtable of Tanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Hoteli ya Hayatt Regency mkoani Dar es salaam, Desemba 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa CEO Roundtable of Tanzania baada ya kuzungumza akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza sekta binafsi kwa namna inavyoshiriki katika kukuza uchumi wa nchi ikiwemo kutoa fursa za ajira kwa Watanzania kupitia makampuni na mashirika mbalimbali nchini.

Ametoa pongezi hizo jana (Jumamosi, Desemba 4, 2021) katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Jumuia ya Watendaji Wakuu wa Makampuni na Mashirika (CEO Roundtable of Tanzania) katika ukumbi wa hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa moja ya mafanikio makubwa ni kuongezeka kwa ajira kutoka ajira milioni 20.5 mwaka 2014 hadi ajira milioni 24.1 mwaka 2020/2021 na kuongezeka kwa ajira kwenye sekta isiyo rasmi kutoka asilimia 22.0 mwaka 2014 hadi asilimia 29.4 mwaka 2020/2021.

Alisema licha ya changamoto ya UVIKO-19, Tanzania imeendelea kufanya vizuri kwenye sekta nyingine za kiuchumi na kutoa ajira katika sekta ya kilimo, hali ambayo inaashiria mwelekeo mzuri katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaolenga kuwa na asilimia 60 ya ajira kwenye kilimo ifikapo mwaka 2025/2026.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uwekezaji, biashara na kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hatua hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uwekezaji nchini hususan kutoka nje ambao kati ya Machi na Agosti, 2021 ulifikia takriban dola za Marekani bilioni tatu.”

Waziri Mkuu alisema Rais Samia ameendelea kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara na anaamini kupitia mkutano huo watatoa ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha shughuli za biashara na uwekezaji.

Aliongeza kuwa Serikali ina matarajio na sekta binafsi kuwa itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na kupunguza hewa ya ukaa na matumizi ya plastiki.

“Ongezeni uwekezaji kwenye miradi ya matumizi ya nishati mbadala, ustawishaji wa misitu na utunzaji wa mazingira na usafirishaji kwa kutumia teknolojia za kisasa zisizozalisha hewa ya ukaa,” alisema na kuongeza:

“Nitoe wito kwenu muendelee kuwaita wawekezaji waje hapa nchini na kuwekeza katika sekta mbalimbali za kilimo, utalii na nishati.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka sekta binafsi iweke kipaumbele na kuzingatia usawa wa kijinsia katika utoaji wa ajira hasa wanawake ili kuunga mkono jitihada za Serikali.

Waziri Mkuu alisema katika mwaka 2020/2021, ukosefu wa ajira kwa wanawake upo juu zaidi ikilinganishwa na wanaume ambapo wanawake wasiokuwa na ajira wanafikia asilimia 12.7 ilhali wanaume ni asilimia 5.8.

“Katika mipango yenu ya sasa na baadaye, toeni kipaumbele kwenye mikakati ya kuwainua wanawake katika shughuli za uchumi na hivyo, kumuunga mkono kwa vitendo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuleta usawa wa kijinsia kwenye maeneo mbalimbali nchini”.

Naye, Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania, Bw. Sanjay Rughani aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyoshirikiana na sekta binafsi katika kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na kuahidi kuwa watahakikisha kupitia shughuli zao, wanaifanya Tanzania ikue kiuchumi siyo tu Afrika bali duniani kwa ujumla.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: