Mwanamuziki Fally Ipupa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini Tanzania kwa ajili ya kufanya Show katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam na baadae ukumbi wa Malaika katika Jiji la Mwanza.
Fally Ipupa akizungumza na waandishi wa habari huku akielekea kwenye gari baada ya kuwasili nchini akitoa Jiji la Paris nchini Ufaransa.
MWANAMUZIKI maarufu wa muziki wa dansi Fally Ipupa amewasili nchini Tanzania akiwa na kundi la zaidi ya wanamuziki 35 kwa ajili ya kufanya maonesho katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam Oktoba 9, 2021 na baadae ukumbi wa Malaila katika Jiji la Mwanza Oktoba 13.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Termina III jijini Dar es Salaam amesema anao uzoefu wa kutosha na wa muda mrefu katika muziki wa dansi,hivyo watanzania watarajie burudani ya nguvu kutoka kwake sambamba na nyimbo zake mpya.
"Nimekuja na vitu vingi vipya, kutakuwa na Suprise , hivyo Watanzania watafurahi sana, niwahakikishi mashabiki wa muziki wa dansi watakaokuja Mlimani City na baadae katika Jiji la Mwanza watafurahi,mimi na wanamuziki wangu tumejipanga,tumejiandaa kutoa burudani, niwaombe tu kateni tiketi mapema, "amesema.
Ameongeza kuwa anatambua hajaja Tanzania kwa zaidi ya miaka 10, hivyo kuna nyimbo nyingi ambazo amezitoa lakini anawaachi mashabiki ndio wataamua wanataka kusikia nyimbo gani kutoka kwake ingawa amejiandaa vya kutosha."Niwahakikishie nitafanya Show ambayo sijawahi kufanya hapa Tanzania,njooni Mliman City siku ya Jumamosi, kutakuwa na Sebene na Rhumba kali."
Kuhusu idadi ya kundi ambalo amekuja nalo ,Fally Ipupa amesema kutoka Paris Ufaransa amekuja na jumla ya watu nane na wengine 24 wataingia usiku wa leo kwa Shirika la Ndege la Ethiopia wakitoa Kinshansa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Prime Time God Kusaga amesema Fally Ipupa tayari amewasili nchini na onesho lake la kwanza litafanyika Jumamosi ya Oktoba 9 katika ukumbi wa Mliman City na baada ya hapo atakwenda Mwanza katika ukumbi wa Malaila Oktoba 13 mwaka huu ambayo itakuwa siku ya mkesha wa Maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Julius Nyerere .
"Maandalizi yamekamilika,tunawaomba mashabiki na wapenzi wa muziki wa dansi,mashabiki wa Fally Ipupa kukata tiketi mapema kwani zimebakia chache kumalizika , tunaamini atafanya Show nzuri na kuutangaza utalii wetu,"amesema Kusaga.
Toa Maoni Yako:
0 comments: