Na Karama Kenyunko wa Globu ya Jamii.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo imemuachia huru mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji na wenzake watatu baada ya Mkurugenzi wa mashtaka ya jinai nchini (DPP) kuwasilisha Nolle Prosequi kuonesha kuwa hana nia ya kuendele kuwashtaki washtakiwa dhidi ya mashtaka yao ya uhujumu uchumi yanayowakabili.

Hakimu Mkazi Huruma Shahidi amewaachia huru washtakiwa hao baada ya DPP kuwasilisha hati hiyo ya kuwafutia mashtaka chini ya kifungu cha sheria namba 91 (1) cha mwenendo wa makosa ya jinai (CPA)

Manji na wenzake watatu, Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), Mtunza stoo, Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43) wameachiwa baada ya kufikishwa mahakamani hapo kwa hati ya wito ya kuwatoa mahabusu (remove order).

Akizungumza mbele ya hakimu Mkazi Huruma Shaidi, wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amesema mahakamani, “tuliomba remove order kwa ajili ya kuwaleta washtakiwa mahakamani hapa kwani DPP kupitia Jamuhuri ameondoa mashtaka dhidi ya washtakiwa na hana nia ya kuendelea kuwashtaki”

Wakili wa utetezi, Hajira Mungula alipoulizwa kama analolote la kusema juu ya hilo, alisema kuwa, “sheria inamruhusu DPP kufanya hayo”. Hakimu Shaidi aliwaambia washtakiwa kuwa wako huru wanaweza kuondoka. “Washtakiwa mko huru ondokeni”.

Manji ameondoka mahakamani hapo akiwa huru bila ya ulinzi wowote akiwa ameongozana na washtakiwa wenzake ha kuingia kwenye gari aina ya Alteza yenye namba za usajili T 383 DFN

Kwa mara ya kwanza Manji na wenzake walisomewa mashtaka hayo ya uhujumu uchumi, July 5 mwaka huu, akiwa kitandani katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo Hospitali ya taifa .

Wote kwa pamoja wanadaikwa kuwa Juni 30, mwaka huu maeneo ya Chang’ombe A wilayani Temeke Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja, walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya Sh milioni 192.5.

Pia inadaiwa Julai Mosi mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A, wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wote walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo nane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ vyenye thamani ya Sh milioni 44.

Katika mashitaka ya tatu, inadaiwa Juni 30, mwaka huu maeneo ya Chang’ombe A, washitakiwa walikutwa wakiwa na mhuri wa JWTZ ambao uliandikwa ‘’Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha JWTZ’’ bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama wan chi.

Pia inadaiwa, terehe hiyohiyo maeneo ya Chang’ombe washitakiwa walikutwa na mhuri uliokuwa umeandikwa ‘’Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama.

Ilidaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo hayo, washitakiwa kwa pamoja walikutwa na mhuri ulioandikwa ‘’Commanding Officer 835 KJ, Mgambo P.o.Box 224 Korogwe isivyo halali.

Katika mashitaka ya sita, inadaiwa Julai Mosi mwaka huu, maeneo hayo ya Chang’ombe, washitakiwa walikutwa na gari lenye namba za usajili SU 383 mali waliyojipatia isivyo halali.

Aidha, wanadaiwa kuwa Julai Mosi mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wote walikutwa na gari lenye namba za usajili SM 8573 pasipo uhalali.

Kabla ya uamuazi huu leo, wiki iliyopita Yusuf Manji na wenzake hao, walipelekwa polisi kuhojiwa kuhusiana na kesi hii ya uhujumu uchumi kwa lengo la kukamilisha upelelezi ambapo walirudishwa baada ya usiku mmoja.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: