Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akizungumza na washiriki wa kongamano la Shirikisho la Vyuo na Vyuo vya Elimu ya juu CCM Zanzibar huko katika hoteli ya Bravo Kiwengwa Mkoa kaskazini Unguja.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Dk. Mohamed Seif Khatib akizungumza katika kongamano hilo.
Baadhi ya vijana wa Shirikisho la Vyuo na vyuo vya elimu ya juu CCM Zanzibar wakishangilia katika shirikisho hilo.
---
Na Is-haka Omar, Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi amewataka vijana wa chama hicho kuchangamkia fursa za kielimu zinazotolewana serikali ili kupata wasomi watakaoendeleza misingi ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa vitendo.

Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza na vijana wa chama hicho katika kongamano la kuwajengea uwezo vijana lililoandaliwa na Shirikisho la Vyuo na Vyuo vya Elimu ya juu CCM Zanzibar, lililofanyika katika hoteli ya Bravo Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kimeweka mikakati endelevu ya kuhakikisha serikali inatoa kipaumbele kwa sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha vijana wanasoma na kupatikana kwa viongozi na wataalamu waliobobea katika fani mbali mbali.

Dk.Mabodi alieleza kwamba mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 waasisi wa CCM walitoa fursa ya elimu kwa kuanzisha mfumo wa elimu bure kwa nia ya kuhakikisha watoto wa wanyonge wanapata elimu ili baadae waweze kujitawala.

“Vijana wa CCM tumieni fursa ya elimu vizuri kwani serikali imeimarisha mfumo wa elimu kuanzia ngazi za maandalizi mpaka vyuo vikuu hivyo hakuna sababu ya kushindwa kusoma.

Maendeleo ndani ya chama chetu yataimarika endapo kutakuwa na vijana makada waliosoma fani mbali mbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa ambao watakuwa na uwezo wa kujenga hoja zenye nguvu zitakazolinda heshima ya chama chetu”, alisema Dk.Mabodi.

Akifungua kongamano hilo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Dk. Mohamed Seif Khatib aliwataka vijana waliopata fursa ya elimu ya juu kuwa wabunifu wa masuala mbali mbali yatakayoweza kuisaidia nchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Alisema matarajio ya Chama cha Mapinduzi na serikali ni kuona vyuo vikuu vinazalisha vijana wenye weledi na uwezo wa hali ya juu katika kuchanganua na kushauri mambo yenye tija na manufaa kwa wananchi wote.

“ Rika la vijana ndio nguvu kazi ya taifa lolote duniani na Chama cha Mapinduzi tunajivunia kuwa tunao vijana waliobobea katika fani mbali mbali hivyo tunaamini kupitia wingi wenu mtaendelea kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo yatakayoweza kuleta manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”, alieleza Dk. Seif.

Dk. Seif aliwataka vijana kuendelea kuwa wazalendo ili chama cha mapinduzi kiweze kushinda na kusimamisha serikali kwa kila uchaguzi mkuu wa Dola.

Naye Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya Mjini, Baraka Shamte ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho, akitoa mada ya Zanzibar ilipotoka, ilipo hivi sasa na inapoelekea alisema historia ya Zanzibar ndio somo pekee litakalowajengea uwelewa mzuri vijana wa sasa.

Alisema kuwa kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 nchi ilikuwa katika dhiki na mateso makubwa yaliyotekelezwa na watawala wa wakati huo dhidi ya wananchi.

Alisema maendeleo yaliyopo nchini yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa CCM wanaosimamia kwa nguvu zote sera za maendeleo na kukuza uchumi kama walivyoaidi kupitia Ilani ya uchaguzi ya chama ya mwaka 2015/2020.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: