Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Inmi Patterson akimkabidhi cheti Paul Alex Sayayu kutoka Asasi Isiyo ya Kiserikali ya ‘Kwetu Faraja’ ya Sengerema, Mwanza kama ishara ya makabidhiano ya fedha za msaada kutoka Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kupambana na VVU/UKIMWI. Vikundi vya kijamii na Asasi Zisizo za Kiserikali 18 ambazo hufanya kazi kusaidia watu walioathirika na UKIMWI vilipata fedha katika sherehe iliyofanyika Ubalozi wa Marekani, jijini Dar es Salaam.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Inmi Patterson amekabidhi fedha za msaada kutoka Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kupambana na VVU/UKIMWI, (AFHR), kwa vikundi vya kijamii na Asasi Zisizo za Kiserikali 18, ambazo hufanya kazi kusaidia watu walioathirika na UKIMWI. Sherehe ya makabidhiano hayo imefanyika ubalozini leo tarehe 6 Septemba, 2017.

Vikundi vilivyopokea mafungu hayo ya fedha viliomba kutoka Mfuko wa Dharura wa
Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) – kwa kuandika miradi ambayo
itasaidia jamii kuthibiti janga la magonjwa hatari kwenye jamii zao wakijikita zaidi katika watu wanaoishi na VVU, wajane, wasimamizi wa familia, makundi maalum yaliyo katika mazingira hatarishi, wakiwamo yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wasichana balehe na wanawake vijana.

Miradi mingi kati ya iliyoorodheshwa hapa chini inalenga kuimarisha upatikanaji wa maji safi, usafi wa afya na mazingira, umeme na mahitaji mengine muhimu katika shule na vituo vya afya. Miradi mingine ni ya shughuli za kuongeza kipato, kama usagaji nafaka na utengenezaji matofali, ikiwa ni njia ya kutengeneza ajira na kuongeza kipato kwa ajili ya wanajamii walio katika hali ngumu. Kwa pamoja miradi hii itasaidia elimu, huduma za afya, na maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania.

Kila mradi unaonesha mfano katika njia ya kufikia wananchi kwa kutokea chini kwenda juu ambapo jamii husika hubainisha matatizo yao na kuja na suluhisho la matatizo hayo. Marekani inaona fahari kushirikiana na watanzania hawa wanaotatua matatizo.

Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kupambana na VVU/UKIMWI (AFHR) ulianza mwaka
2009 na umekwishatoa fedha kwa vikundi vya kijamii 93 hapa Tanzania. Mpango huu
umeendelea kuwa utamaduni imara wa ushirikiano kati ya wananchi wa Marekani na Tanzania.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: