Jumanne, Novemba 1, 2016-Kulia ni meneja wa mgodi wa dhahabu wa Acacia Buzwagi uliopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga Asa Mwaipopo akimkabidhi mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu mashine maalumu ya ufuatiliaji wa mapigo ya moyo ya mgonjwa kwa ajili hospitali ya halmashauri ya mji wa Kahama.
---
Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Acacia kupitia mgodi wake wa Buzwagi imekabidhi vifaa tiba vya kisasa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi 22,410,000/= kwa hospitali ya halmashauri ya mji wa Kahama kwa ajili ya kuisaidia katika kuboresha huduma zake za fya kwa jamii.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni mashine tatu maalumu za oksijeni,viti vitano vya magurudumu kwa ajili ya wagonjwa,machela mbili za kisasa zenye magurudumu,mashine maalumu ya ufuatiliaji wa mapigo ya moyo ya mgonjwa na mashine mbili maalum za umeme za kusafishia vifaa vya upasuaji.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa hospitali hiyo, meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo alisema wametoa msaada huo baada ya uongozi wa Acacia kutembelea hospitali hiyo na kujionea mapungufu ya vifaa tiba.
“Kutokana na kwamba kuwajibika kwa watu wetu na jamii inayozunguka imekuwa utamaduni wetu,tulifanya kikao na baadhi ya viongozi wa hospitali hii,walionesha nia ya kuhitaji msaada ili kukabiliana na changamoto za tiba”,alieleza Mwaipopo.
“Kama sehemu ya mpango wa sera yetu ya mahusiano ya jamii,leo tunakabidhi vifaa hivi ambavyo tunaamini vitasaidia kupunguza changamoto mbalimbali za tiba kwa wagonjwa na kuleta ahueni kwa wagonjwa na pia vitawasaidia madaktari waweze kutoa huduma kwa wagonjwa wengi zaidi ili kuokoa maisha ya watu wengi zaidi”,aliongeza Mwaipopo.
Akipokea msaada huo,mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu mbali na kuupongeza mgodi wa Buzwagi kwa msaada huo,pia aliwataka viongozi wa hospitali hiyo kutunza vifaa hivyo vya kisasa na kutumia kwa matumizi yanayotakiwa kwani wananchi wengi wanahitaji huduma.
Naye mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Kahama Dkt. Bruno Minja aliushukuru uongozi wa Buzwagi kwa msaada huo ambao umelenga moja kwa moja kuboresha huduma kwa wagonjwa na kurahisisha utoaji huduma kwa watoa huduma.
Minja alisema watavitumia vyema vifaa hivyo hususani katika huduma ya mama na mtoto,huduma za upasuaji na huduma za dharura ikiwemo ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikijitokeza.
Toa Maoni Yako:
0 comments: