Waziri Sitta akiongea na waandishi wa habari jijini Dar waakati akiangaza kumsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya bandari.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam. 

Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande baada ya kuwepo malalamiko ya ubabaishaji katika zabuni mbalimbali za mamlaka hiyo.

Hatua hiyo ya Sitta imekuja wiki tatu baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuiongoza wizara hiyo akitokea Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla, wizara hiyo ilikuwa chini ya Dk Harrison Mwakyembe.

Sitta, ambaye pia hujulikana kama Mzee wa Viwango, amewaambia waandishi wa habari jijini kuwa wadau mbalimbali wamesema taratibu za zabuni TPA haziendeshwi kwa uwazi na uaminifu.

“Wanasema hakuna uwazi katika zabuni, kuna dalili ya ubabaishaji. Katika kamati za kutathmini zabuni majina ya watu yanabadilika badilika na hata baada ya mshindi kupatikana bodi huchelewa kutoa barua inayohusu uamuzi wa kumpata mshindi huyo,” amesema Sitta.

“Hayo yote yanajenga taswira isiyo nzuri kwa bandari, serikali na nchi nzima kwa ujumla,”

Kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za bandari, amesema ameamua kumsimamisha Kipande kupisha uchunguzi kwa kipindi hicho na nafasi yake itachukuliwa na Meneja Bandari ya Dar es Salaam, Awadh Massawe.

Kutokana na kusimamishwa kwa kigogo huyo, Sitta aliitangaza tume maalumu ya watu sita itakayochunguza tuhuma hizo ikiongozwa na Jaji Mstaafu Augusta Bubeshi na itafanya kazi hiyo kwa majuma mawili.

Wengine katika tume hiyo ni Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) Dk Ramadhan Mlinga, Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa TPA Samson Luhigo, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu, TPA Happiness Senkoro.

Pia, katika tume wapo Mkurugenzi wa Masoko mstaafu wa TPA Flavian Kinunda na Mtumishi wa Wizara ya uchukuzi Deogratius Kassinda atakaye kuwa Katibu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: