Tigo Tanzania imepanga mwaka huu kujenga minara 10 mipya ya simu yenye thamani ya dola milioni moja (1) katika visiwa vya Zanzibar kama moja ya mikakati yake ya upanuzi wa huduma zake nchini.

Hii ilitangazwa leo na Kaimu Meneja Mkuu mpya wa Tigo Bi. Cecile Tiano wakati alipotembelea Zanzibar kwa mara ya kwanza kukutana na wadau wa kampuni kisiwani hapo.

Bi. Tiano alisema kwamba minara hii mipya 10 ni uwekezaji mkubwa ambao kampuni hiyo imewahi kufanya ndani ya mwaka mmoja katika kisiwa hicho ukilinganisha na mwaka uliopita ambapo Tigo ilijenga mnara mmoja. Tigo inajumla ya minara 51 Zanzibar, kutokana na maelezo ya Kaimu Meneja Mkuu huyo.

"Baadhi ya minara hii mipya itatoa huduma ya kasi ya intanet ya 3G inayomaanisha upatikanaji zaidi wa data kwa wateja wetu na watalii wanaotembelea kisiwa hiki. Upatikanaji huu zaidi wa intanet tunaamini utapelekea kuongezeka kwa muingiliano wa utandawazi baina ya Zanzibar na mataifa mengine utaleta fursa mpya za kijamii na kiuchumi kwa ajili ya watu wa Zanzibar," Bi. Tiano alisema.

Alisema kwa upande wa nchi nzima, Tigo itawekeza katika minara mipya 748 yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 75 ikiwa inalenga kufikia maeneo ya vijijini, "wakiwa na huduma zinazofurahisha kama Facebook ya Bure kwa Kiswahili, Tigo Music na mengineyo," alisema.

Bi. Tiano aliahidi kwamba kampuni ya Tigo itaongeza kiasi cha misaada na uwekezaji katika jamii na shughuli za maendeleo katika maeneo ya elimu, afya, TEHAMA, watoto na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake, huku akikumbusha mchango wa kampuni hiyo uliotoa kwa kisiwa hicho mwaka 2014 ambao ulijumuisha msaada wa madawati na kompyuta kwa shule za sekondari na misingi, utoaji wa mashine za kutengeneza mwani kwa wakulima wa Pemba na msaada wa vifaa vya kisasa vya kilimo kwa wakulima wa Zanzibar, vyote vyenye thamani ya shilingi milioni mia moja (100).

"Tunafanya hivi, tukiamini kwamba kama kampuni ya kizawa, ni jukumu letu kuendelea kufanya kazi na washiriki wetu binafsi pamoja na serikali kutoa suluhu ambazo zinalenga kutatua changamoto za kijamii zinazoweza kuchochea maisha bora na maendeleo ya kiuchumi kwa mapana yake," alisema.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: