Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika mazungumzo na kiongozi wa Rais wa kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) duniani, Dkt. Ted N.C. Wilson aliyemtembelea pamoja na ujumbe wake wa viongozi wa kanisa hilo kutoka nchi 11 za Afrika Ikulu Jumamosi February 7, 2015, Usiku jijini Dar es salaam.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo na kupata chakula cha usiku na kiongozi wa Rais wa kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) duniani, Dkt. Ted N.C. Wilson aliyemtembelea pamoja na ujumbe wake wa viongozi wa kanisa hilo kutoka nchi 11 za Afrika Jumamosi February 7, 2015, usiku Ikulu jijini Dar es salaam. PICHA NA IKULU
Na Mwandishi Wetu.
Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) duniani limeipongeza Tanzania na Watanzania kwa kulinda amani nchini na pia kusaidia kuleta na kuinua kiwango cha amani na utulivu katika nchi nyingine katika eneo la Mashariki na Kati la Afrika.
Aidha, Kanisa hilo limepongeza msimamo na sera ya Serikali ya Tanzania ya kuvumilia na kulinda uhuru wa watu kuabudu dini yoyote waitakayo na kamka mtu anataka kuamua kutokuwa na dini.
Pongezi hizo kwa Tanzania zilitolewa usiku wa jana, Jumamosi, Februari 7, 2015, na Kiongozi wa Kanisa hilo la SDA duniani, Rais wa the General Conference of the Seventh Adventist Church, Dkt. Ted N.C. Wilson na viongozi wenzake wakiwemo kutoka nchi za Afrika 11 wakati walipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, na baadaye kula naye chakula cha usiku Ikulu, Dar Es Salaam.
Katika mazungumzo na Rais Kikwete na baadaye wakati wa hotuba yake kwenye chakula, Dkt. Wilson alimwambia Rais Kikwete: “Nataka kukupongeza na kukushukuru sana kwa kudumisha amani katika Tanzania na katika nchi nyingine za Afrika.”
Aliongeza: “Historia yako na ile ya Tanzania katika eneo hili inajulikana duniani pote. Hakuna shaka kuwa mmefanya juhudi kubwa kulinda na kudumisha amani hapa kwenu na nje ya nchi yenu. Kwetu sisi amani na utulivu ni mambo muhimu kwa sababu yanasaidia kueneza neno na injili ya Mungu katika hali salama kabisa.”
Kiongozi huyo wa SDA aliongeza: “Aidha, tunakushukuru sana wewe na kuipongeza sana nchi ya Tanzania kwa uvumilivu wa imani za kidini na pia kwa kuweka, kulinda na kudumisha uvumilivu na uhuru wa kuabudu ambako kila mtu ana haki ya kuamua anaabudu nini. Asante, Mheshimiwa Rais na nchi yako, kwa kuinua kiwango cha uhuru na uvumilivu.”
Dkt. Wilson na viongozi wa SDA kutoka nchi mbali mbali duniani walikuwa nchini kushiriki katika mkutano wa kidini ujulikanao kama Blessings in Mission East and Central Africa ambao ulifanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar Es Salaam.
Dkt. Wilson alimweleza Rais Kikwete kuwa Kanisa lake limefanya mkutano mzuri na wa kuvutia na kuwa inakadiriwa kuwa kiasi cha watu 40,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania walishiriki mkutano huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: