Wapendwa natamani tuitumie kwaresma hii kutafakari kidogo kuhusu ubinadamu, na ikiwezekana tuimarishe namna yetu ya kuwachukulia binadamu wenzetu.
Mambo mengi tunayoona yanatuudhi kwa wenzetu ni ya kibinadamu na lazima wawe nayo ili wasiwe sawa na Mungu.
Ndiyo hayo yaliyofungwa kwenye ile miti miwili ya katikati ya bustani ya Eden. Yaani mti wa uzima (ambao awali tuliruhusiwa kuula), na mti wa ujuzi ambao tulikatazwa kuula tukafanya kiburi.
Ikumbukwe kwamba baada ya kula matunda ya mti wa ujuzi, tulifukuzwa kabisa bustanini na Mungu akaweka walinzi ili tusirudi kamwe kuyala matunda ya miti yote miwili.
Kuzuiliwa kula matunda ya mti wa uzima kukasababisha kuanzia hapo mwanadamu awe anakufa. Na kuzuiliwa kuendelea kula mti wa ujuzi kukasababisha tujue mema na mabaya kwa kiasi fulani tu kwa sababu tulikwishadokoa matunda yale, lkn tukabaki tunafanya mambo kadhaa bila kujijua wala kujitambua wala kuweza kujizuia kwa sababu hatukupata fursa kuendelea kula matunda ya ujuzi hivyo ujuzi wetu ukawa wa kiasi fulani tu.
Hakuna kati yetu anayepanga kwamba sasa ngoja nichoke, au akajipimia nichoke kwa kiasi hiki, au akasema nimeamua nichoke. Uchovu ni hulka halisi ya mwanadamu isiyoepukika, hivyo siyo sahihi kumkasirikia mtu au kumwona dhaifu kwa sababu amechoka.
Hulka nyingine za namna hii ni kama vile hasira, kujisahau, kuhamaki/kupaniki, njaa, kiu, hamu, kunogewa, kujitetea/kujieleza, kuhisi usumbufu, nk.
Ubinadamu huu hauepukiki, hivyo yafaa kila mmoja aheshimu ubinadamu wa mwingine.
Hulka za kibinadamu zilipata heshima zaidi pale ambapo Mungu mwenyewe alizivaa na kuziishi hizo hizo. Cha ajabu Mungu alipoziishi tunapaheshimu, lkn wenzetu wakiziishi tunaowana wadhambi na kuwachukia.
Tukumbuke Mungu baada ya kuumba kila kitu hata kusiwepo chochote ambacho hakikuumbwa naye, akaamua pia kuwa mtu. Hivyo akawa MUNGU KWELI NA MTU KWELI.
Tukasome Yohane 1:1-14.
Na alipokuwa mtu kweli, alikabiliwa na changamoto zote ambazo binadamu wenzake tunakabiliana nazo. Hulka za kibinadamu zilimzonga kama sisi wenzie, ila tu yeye hakutenda dhambi. Tunasoma:
"Alijaribiwa sawa sawa na sisi kwa kila jambo, isipokuwa yeye hakutenda dhambi" Ebr. 4:15
Tuangalie mifano michache ya hulka za kibinadamu alizokuwanazo Yesu ambazo kwake tunaziona ni njema, lakini kwa wengine tunawaona ji wapuuzi na hawafai.
1. Yesu aliona kiu.
- Aliomba maji ya kunywa kwa mama Msamaria, Yohana. 4:7
- Alilia kwamba anakiu pale msalabani, Yohana 19:28
2. Yesu alihisi njaa
- alikula ngano za watu yeye na wafuasi wake, na akajitetea kwamba hata babu yake (mfalme Daudi) na watu wake walipopata njaa walivamia mikate ya hekalu. Mt. 12:3
Leo wewe ukihisi njaa ukamwomba mwenzio akudomdoshee punje chache za karanga anazokula moyoni atakuhisi kuwa mlafi na huwezi kujizuia.
- Alipofunga Jangwani alipata njaa kali. Mt. 4:2
3. Alikasirika
- Alipanda jazba na kuwatandika viboko waliokuwa wanauza bidhaa hekaluni, ikiwa ni pamoja na kuvunjavunja meza zao.
Leo wewe ulikasirika ukawakemea waliochelewa mazoezini utaitwa mbabe na mjuaji.
4. Alinogewa na kujisahau
- alinogewa na darasa la torati na akajisahau kwa siku tatu bila wazazi wake kujua huku wakihangaika kumtafuta.
Tusome Luka 2:44-46
Leo wewe ukijisahau kidogo utaitwa mzembe, taahira, zoba.
5. Alihusudu undugu, ujamaa
- kabla ya kufa alitangaza undugu kati ya mama yake na mfuasi aliyempenda. Yohana. 19 : 25-27
Leo wewe ukimjali binadamu unaambiwa unaendekeza undugu ndiyo maana hutaendelea
6. Alihisi usumbufu
- mama yake alipomtuma akaonesha kwamba anasumbuliwa hata akamwuliza "tuna nini mimi na wewe mama?"
Tusome Yohana. 2:4
Leo wewe ukionyesha hisia za kukumbuka utahesabiwa jeuri na mwenye kiburi.
7. Ali-jistify/ alijieleza/alijitetea
- Baada ya kukutwa hekaluni na wazazi wake waliomtafuta sana aka - justify na kuwaambia haikuwa lazima Kwao kuhofia.
Leo wewe ukijieleza unaambiwa mbishi na unapenda kujitetea sana.
8. Alipaniki
- alipoona mateso yamekuwa makali, alipaniki na akahisi hapewi msaada ambao aliamini alistahili kupewa. Akahisi ametelekezwa na hakumwelewa Mungu kwa sababu hakutarajia kama angeweza kumtelekeza.
Hata akamwuliza kwa sauti na kilio,
"Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? " Mt. 27:47
Leo wewe ukipaniki na kuingia hofu utaambiwa huna imani. Ukihisi kuachwa utaambiwa unakata tamaa.
Wapendwa, mifano hii michache itukumbushe kwamba binadamu tunaishinao wana hulka kamili za kibinadamu. Tusiwe wepesi kuwashangaa au kiwahukumu pale hulka zao zinapojidhihirisha. Tuwachukulie kwa upendo tukikumbuka kwamba ndiyo asili yetu sote.
Hii itatusaidia kupiga hatua katika yafuatayo :
i. Hatutakwazika kwa mambo madogo madogo watendayo wenzetu. Nafsi zetu zitabaki na amani wakati mwingi.
ii. Tutasamehe kwa urahisi sana. Tutakuwa na roho nyeupe wakati mwingi
iii. Tutawasaidia wenzetu kirahisi kubeba mizigo yao. Watatuona rafiki na tumaini lao, uhusiano wetu utakuwa mzuri wakati mwingi
iv. Tutatambua kwamba na sisi tu dhaifu, hivyo tutajitahidi kushinda udhaifu wetu, na hatutakasirika wenzetu wakitushauri au kutukumbusha kufanya marekebisho au maboresho fulani.
Watatuona watu wema na watakuwa huru kwetu. Uhusiano wetu utakuwa wa kudumu zaidi.
Nawatakieni kwaresma njema.
Tumsifu Yesu Kristo. .
Toa Maoni Yako:
0 comments: