Picha namba 06534 ni Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani almaarufu Maji Marefu akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya watoa huduma ya mradi wa KFW waliosajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Mamba wilayani Korogwe.
Washiriki wa mafunzo ya watoa huduma ya mradi wa KFW waliosajiliwa na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) kutoka Halmashauri mbalimbali mkoani Tanga wakifuatilia kwa umakini mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye mafunzo hayo jana yanayofanyika kwenye ukumbi wa Mamba wilayani Korogwe. Picha na Oscar Assenga

NA MWANDISHI WETU, KOROGWE.

ZAIDI ya bilioni 6 zimetumika kuwalipia wakina mama wajawazito na watoto katika vituo mbalimbali vya afya katika mikoa ya Tanga na Mbeya ambao ni wanachama na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kupitia mradi wa (KFW).

Mradi huo unaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Benki ya Maendeleo ya watu wa Ujerumani (KFW) ambao unatekelezwa hapa nchini katika mikoa ya Tanga na Mbeya.

Hayo yalibainishwa kwenye ufunguzi wa mafunzo ya watoa huduma wa mradi wa (KFW) juzi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,Daudi Bunyinyiga ambapo alisema kwa kiasi kikubwa mradi huo umevuka lengo la walengwa waliokusudiwa awali kuandikishwa katika mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) kupitia mradi huo.

Alisema kuwa wakati mradi huo ulipoanzishwa ulitarajiwa kuwahudumia akina mama wajawazito 80, 0000 katika kipindi cha miaka mitatu ya mradi huo wakati mpaka sasa umeandikisha na kuwahudumia akina mama wajawazito 190,631 kwa mikoa ya Tanga na Mbeya hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 238.

Bunyinyiga ambaya pia ni Meneja wa Miradi inayosaidiwa na wahisani alisema kuwa kwa mkoa wa Tanga fedha zilizotumika zilizokuwa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 958 ambapo mradi huo umeweza pia kutumi kiasi cha shilingi milioni 989.1 kwa ajili ya kununulia vifaa tiba ikiwemo vitanda vya kujifungulia, mashine za kutakasia vifaa zilizovyokwisha kugawiwa kwa mikoa ya Tanga na Mbeya.

Akizungumzia kuhusu mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) alisema kuwa Jumla ya Shilingi bilioni 1.5 zimelipwa katika Halmashauri mbalimbali ili kuwaandikisha akina mama hao na familia zao katika mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Alisema kuwa lengo la kuwaandikisha akina mama hao na familia kwenye (CHF) ni kuhakikisha wanapata huduma endelevu baada ya kumalizika kwa muda wa kupata huduma katika mfuko wa Bima ya Afya ambapo huduma hizo ni kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Katibu Tawala wilaya ya Korogwe Stanley Lameck ambaye alimuwakilisha Katibu tawala mkoa wa Tanga,Salum Chima alisema kuwa mpango huo wa KWF kwa mkoa umekuwa na mafanikio makubwa hasa ukizingatia kuwa kundi la walengwa wa awali wanawake na wototo ndio waliokuwa na changamoto kubwa ya huduma za matibabu tangu hatua za mwanzo za ujauzito hadi kujifungua.

Alisema kuwa kupitia mradi huo idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vyakutolea huduma imeongezeka kutoka asilimia 48 mwaka 2011 hadi zaidi ya asilimia 60 mwaka 2013.

Hata hiyo alisema kuwa vifo vya wakina mama vinayotokana na matatizo ya uzazi wakati wa kujifungua vimepungua kutoka 110 mwaka 2013 hadi kufikia 69 kwa mwaka 2014 ikiwemo kwa watoto wachanga chini a mwezi mmoja kutoka 275 kwa mwaka 2013 hadi kufikia 206 mwaka 2014.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: