RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika juhudi za kuhakikisha uwepo wa madaktari bingwa wa fani mbali mbali wakiwemo wanaohusiana na maradhi ya mfumo wa utoaji wa haja ndogo katika kipindi kifupi kijacho.

Dk. Shein aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Breezes iliyoko Bwejuu Mkoa wa Kusini Unguja, katika mkutano maalum wa wataalamu wa maradhi yanayohusiana na mfumo wa utoaji wa haja ndogo kutoka Uingereza ambao kwa mwaka huu wameichagua Zanzibar kuwa ni sehemu ya kufanyia mkutano wao.

Mkutano huo pia, umehudhuriwa na madaktari bingwa wa maradhi hayo kutoka Tanzania Bara, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Jumuiya hiyo kwa kuamua kufanya mkutano huo hapa Zanzibar huku akieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwapata wataalamu wakiwemo wa maradhi yanayohusiana na haja ndogo na maradhi mengineyo.

Alisema kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa lengo la kupata Madaktari ili kuongeza utoaji huduma kwa wananchi ambapo kwa hivi sasa Daktari mmoja amekuwa akitibu watu 9,708.

Katika kuhakikisha idadi ya Madaktari inaongezeka Dk. Shein alisema kuwa kwa kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kukiimarisha Chuo chake cha Madaktari ambacho hivi sasa kina wanafunzi 99 wanaosoma kwa mwaka wa kwanza na wa pili.

Aidha, alisema kuwa Serikali inakiimarisha Chuo chake cha Afya kilichopo Mbweni Zanzibar ambacho kinatarajiwa kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) pamoja na kuhakikisha Hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmmoja inafikia lengo lililowekwa sambamba na ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Mkoani Pemba unaoendelea.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo, kutoa shukurani kwa juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya ya Misaada ya Uingereza ya Uimarishaji wa programu za Afya hapa Zanzibar (HIPZ), kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutoa na kuimarisha huduma hizo katika hospitali za Makunduchi na Kivunge. “Natumia fursa hii kutoa shukurani kwa Dk. Ru McDonagh na madakatari wote kwa huduma wanazozitoa katika hospitali hizi....”,alisema Dk. Shein.

Aidha, alisema kuwa kuimarisha huduma za afya ni miongoni mwa vipaumbele vikuu vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi za kupunguza umasikini katika jamii licha ya baadhi ya changamoto zilizopo ambazo kwa juhudi za pamoja na kwa mashirikiano ya washirika wa maendeleo ufumbuzi wake utapatikana.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio yaliopatikana katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sera katika sekta hiyo huku akieleza azma ya Serikali anayoiongoza kuangalia uwezekano wa kutoa huduma bure za afya kama ilivyotangazwa mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Zanzibar na hatimae Aprili 26, 1964 ilipojiunga na Tanganiyika na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kutoa historia katika sekta ya afya hapa nchini kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, baada ya Mapinduzi na hatua zinazochukuliwa hivi sasa.

Nao Madaktari bingwa wa maradhi ya mkojo walioshiriki katika mkutano huo wakitoa mada mbali mbali ikiwa ni pamoja na hatua zinazochukuliwa na Jumuiya hiyo kutoka Uingereza ya kitengo cha maradhi ya haja ndogo katika kuyatafutia ufumbuzi maradhi hayo nchini Uingereza sambamba na mafanikio yaliofikiwa.

Aidha, Madaktari hao walieleza historia ya maradhi hayo pamoja na kuonesha juhudi zilizochukuliwa nchini Uingereza tokea miaka ya 1800 pamoja na namna ya kutafuta tiba sambamba kuonesha tafiti mbali mbali zilizofanywa na Madaktari bingwa wa nchi hiyo.

Madaktari hao, walipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kuunga mkono azma ya Serikali katika kuhakikisha wataalamu wa kutosha wa maradhi hayo katika kipindi kifupi kijacho wanapatikana hapa Zanzibar.

Nae Dk. Roger Plail, akitoa neno la shukurani kwa Dk. Shein alieleza kufarajika kwao na uamuzi wa kuja Zanzibar kufanya mkutano huo wa wataalamu kutokana na mashirikiano mazuri yaliopo kati yao na Madaktari wa Zanzibar akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Saleh Mohamed Jidawi pamoja na uongozi wa Hospitali ya Mnazimmoja.

Kwa niaba ya Madaktari hao Dk. Plail alimpongeza Dk. Shein ambaye ni mtaalamu katika fani ya Patholojia, kwa kuwapa maelezo ya kina juu ya sekta ya afya hapa nchini, historia yake pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana huku wakitoa shukurani kwa mwaliko rasmi aliowapa wa chakula cha mchana hapo kesho (Ijumaa Januari, 22 mwaka huu) Ikulu mjini Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: