Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emanuel Mjema (wa pili kutoka kulia) akiwatambulisha viongozi wa chuo cha CBE kwa Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd (katikati) leo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya chuo hicho kutimiza miaka 50. Kulia ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd akipata maelezo kutoka kwa Bi. Esther Kibua, mwanafunzi wa mwaka wa 3 wa chuo cha Elimu ya Biashara CBE kampasi ya Dar es salaam juu ya namna chuo hicho kinavyowaandaa kuitumia elimu wanayoipata chuoni hapo pindi watakapomaliza masomo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd akimuuliza swali Bi. Esther Kibua, mwanafunzi wa mwaka wa 3 wa chuo cha Elimu ya Biashara CBE kampasi ya Dar es salaam alipotembelea banda la maonesho la wanafunzi wa Chuo cha CBE leo jijini Dar es salaam wakati wa sherehe za kilele cha miaka 50 ya chuo hicho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd akifafanua akifafanua jambo alipotembelea banda la maonesho la Idara ya Mizani na Vipimo la Chuo cha CBE leo jijini Dar es salaam wakati wa sherehe za kilele cha miaka 50 ya chuo hicho.Kushoto ni Mwalimu wa Idara ya Mizani na Vipimo wa Chuo hicho Bw. Faraja Nyoni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd akiwahutubia wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe sherehe za miaka 50 ya CBE leo jijini Dar es salaam.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd akiwa katika picha ya pamoja na Bodi ya uongozi na Menejimenti ya CBE. Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.

Na Aron Msigwa – MAELEZO Dar es Salaam.

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd ameugana na wasomi mbalimbali, viongozi wa Serikali, wanafunzi na wananchi kuadhimisha miaka 50 ya Chuo cha elimu ya Biashara (CBE) tangu kilipoanzishwa mwaka 1965.

Maadhimisho hayo yamefanyika leo jijini Dar es salam, katika viwanja vya chuo hicho na kutoa fursa ya mgeni rasmi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd kutembelea mabanda ya maonesho yaliyokuwepo chuoni hapo ili kujifunza na kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi wa chuo hicho.

Akiwahutubia wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo Balozi Idd ametoa Pongezi kwa uongozi wa chuo hicho kwa kuendelea kusimamia viwango vya taaluma zinazotolewa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za uhaba wa vyumba vya mihadhara na miundombinu isiyotosheleza mahitaji halisi ya chuo.

Balozi Idd amesema kuwa Serikali itaendelea kukijengea uwezo chuo hicho ili kiweze kukidhi matarajio ya wananchi ya kuendelea kuwa chuo bora kinachozalisha wataalam wa fani mbalimbali huku akiahidi kukisaidia kupata dhamana ya Serikali ili kiweze kukopa fedha kutoka katika taasisi za kifedha kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu yake.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Emanuel Mjema akizungumza wakati wa kuwakaribisha wageni mbalimbali chuoni hapo amesema chuo hicho sasa kinafurahia matunda ya mafanikio ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake .

Amesema yapo mabadiliko na maboresho makubwa yaliyofanywa na chuo hicho hasa ongezeko la udahili wa wanafunzi, ongezeko la fani za masomo na kampasi za chuo hicho kutoka 1 iliyokuwepo mwaka 1965 mpaka 4. Zilizopo Dar es salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya.

Prof. Mjema ameeleza kuwa chuo cha CBE sasa kinatimiza miaka 50 kikiwa chuo pekee Afrika ya Mashariki na katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kinachotoa wanafunzi wa shahada ya vipimo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere , chuo hicho kimepata mafanikio makubwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka kutoka wanafunzi 25 mwaka 1965 hadi 14,000 mwaka 2014.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi kufikia shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada za uzamivu (PhD) chuoni hapo pamoja na chuo kuanzisha ushirikiano wa elimu na vyuo vikuu vingine nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Eastern Finland katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia TEKNOHAMA kwa nchi za SADC.

Aidha, katika kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi na kuendana na mahitaji na mabadiliko ya kiuchumi yanayotokea nchini kuanzia mwaka ujao kitaanza kutoa mafunzo ya shahada ya uzamili katika masuala ya Gesi na Petroli.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: