Siku moja nilikuwa nasikiliza wimbo mmoja wa Malkia wa Mipasho Bi Khadija Kopa, alikuwa anawapasha wakuja kuwa wasije na majembe mjini watalima lami. Nikacheka sana na kujiuliza fala gani atakuja mjini kulima lami? Si atakufa kwa njaa jamani.
Sasa juzi nimebadili mawazo, nimegundua kumbe kulima lami ni bonge ya dili. Kuna kabarabara fulani kako mitaa ya ndani ndani kule Kijitonyama Dar es Salaam mjini. Haka kabarabara kama miezi sita iliyopita hivi kakafungwa kama wiki kadhaa kakapakwa lami.
Miezi miwili badae lami si ikaanza kubanduka, lile bonge la mvua lililoanguka baada ya hapo ndio likafuta kabisa kale kalami. Si ndio likaja hili dili la kulima lami.
Jamaa flani wakaanza kufunga barabara upande mmoja wanalima lami kwa siku mbili tatu kisha wanafungua barabara upande huo wanafunga upande mwingine wanaendelea kulima lami huko, ushafika mwezi wa pili sasa gemu hilo linaendelea, vibarua na vijamba koti vya rangi za kung’aa wanalipwa kwa kulima lami, lazima aliyewaajiri anachukua mpunga mzito, toka kwa wenye barabara.
Jamaa hawa wakitaka kokoto za kujaza walipolima, wanakodi hivi visuzuki vilivyokaa kama viloli vya kuchezea, ambavyo madereva wake wanaendesha utadhani wanaendesha vibajaji, wanakodi halafu wanaenda kuomba kokoto sehemu kuna mtu kamaliza ujenzi, wanakuja fukia pale walipolima.
Kwa hiyo na mimi hili dili sitaki linipite, nina mpango wa kununua majembe manne, sululu mbili, na vile vijamba koti vyenye rangi ya kung’aa vinne, nikipata hivyo naanzisha kampuni natafuta kazi ili nami niwe naingiza mkwanja kwa kulima lami. Hili dili liko wazi kabisa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: