Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Serikali ya Tanzania imeendelea kuweka misingi imara ya kufanyiakazi maoni ya wananchi kuhusu hali ya utawala bora nchini kama yalivyobainishwa kupitia Ripoti ya Hali ya Utawala Bora iliyoandaliwa na Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Itakumbukwa kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi 34 kati ya 54 za AU zilizokwishajiunga na Mpango wa APRM. Tanzania ilijiunga na mchakato huu mwaka 2004 na Bunge kuridhia mnamo tarehe 1 Februari 2005.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Mei 11, 2014 na APRM Tawi la Tanzania, imeeleza kuwa tayari Wizara mbalimbali zilizoguswa na Ripoti hiyo zimekwishakuelekezwa kufanyiakazi changamoto zilizobainishwa na kutoa taarifa.

“Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuiwasilkisha Ripoti ya Tanzania mbele ya Wakuu Wenza wa Nchi za APRM mwaka jana, Serikali ilitakiwa kuanza kufanyiakazi changamoto za kiutawala bora zilizobainishwa.

“Utekelezaji huo unaendelea vyema. Masuala mengi ya kikatiba yameingizwa kwenye rasimu inayojadiliwa. Masuala ya kisera na kitaasisi tayari yamefikishwa katika taasisi husika kwa ajili ya kufanyiwakazi,” ilisema taarifa hiyo.

APRM ni nyenzo mojawapo ya kutathmini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa shughuli za maendeleo na ujenzi wa utawala bora kote Barani Afrika ikiwemo Tanzania katika ili kutafakari kwa pamoja namna bora Zaidi ya kuziendeleza juhudi hizo.

“Mpango huu wa kujithamini Kiutawala Bora ni muhimu kwetu na unaakisi Sera zetu na za Waasisi wa Taifa hili juu ya Kujikosoa na Kujisahihisha. Aidha, unahusisha Viongozi wa Afrika na unatoa fursa kwa wananchi kutathmini hali ya utawala bora katika nchi zao na kuendeleza dhamira ya serikali ya uwazi na ujenzi wa pamoja wa utawala bora nchini kwa kuwashirikisha Wananchi wake,” imesisitiza sehemu ya taarifa hiyo.

Ripoti ya APRM Tanzania ambayo itatumika kama rejea muhimu, imeeleza kwa kina juhudi za Tanzania katika kulinda amani. kuimarisha utawala bora na wa sheria na jitihada katika kulinda haki za binadamu.

Hata hivyo Ripoti hiyo pia imegusia changamoto zinazopaswa kufanyiwakazi ambazo ni suala la kushughulikia kero za Muungano, kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo, kuimarisha zaidi juhudi za kuondoa umaskini na kuilinda amani ya nchi na ujenzi wa utawala bora.

Kuhusu mchakato wa sasa wa Katiba unaendelea taarifa hiyo imesisitiza: “Tumeaswa kuutumia vyema mchakato wa sasa wa Mabadiliko ya Katiba kuijenga Tanzania bora zaidi katika miaka mingine mingi ijayo.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: