MOJA ya vibao gumzo katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini kwa sasa ni ‘Kipi Sijasikia’, cha mkali wa Hip Hop Afrika Mashariki na Kati, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ alichomshirikisha nyota wa Bongo flava, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Ni mwezi mmoja sasa tangu Profesa Jay alipoutambulisha wimbo huu, uliobeba mistari ya uzani wa juu, kama ilivyo kawaida ya mkali huyu anayetambulika pia kwa majina ya The Heavyweight MC, Profesa Jiize, Daddy, nk.

Tofauti na vibao vyake vingi vilivyotangulia ambavyo amefanya simulizi kadhaa za kusadikika na kuteka hisia za wengi, ‘Kipi Sijasikia’ ni mkusanyiko wa kilio cha kweli juu ya yale aliyozushiwa kwa nyakati tofauti.

Walishazusha nimekufa, eti nimepata ajali
Washindwe na walegee, Mwenyezi niepushie mbali
Wakasema nina ukimwi kwa kuwa nilikonda ghafla
Wanataka kunizika mzima kabla sijafa
Waliosema nina ‘ngoma’ wengine tushawafukia
Wanaoomba nife leo naamini watatangulia
Ni baadhi ya mistari aliyoimba Jay katika ubeti wa pili wa ‘Kipi Sijasikia’, kibao chenye beti tatu zilizobeba mistari 48 iliyokusanya kila baya lililosemwa kuhusu yeye, 20 kati ya hiyo ikiwa katika ubeti wa kwanza, 16 ubeti wa pili na 12 ubeti wa mwisho.

Jay hajaishia kulalamikia mabaya aliyozushiwa tu, bali ameenda mbali kwa kuwaombea kwa Mungu waliojiua kwa masimango, huku akimsihi Mola wake kuendelea kumpa ujasiri hadi kifo chake na kuwajaalia nguvu waliokata tamaa.

Mungu walaze pema waliosemwa wakajiua
Ingawa wote tunapita naamini maisha ni hatua
Maneno ya watu sumu yanaponya na yanaua
Please, nipe ujasiri mpaka siku ukinichukua
Wape nguvu wale wote waliokata tamaa
Maneno yanaleta hila na mzozo kwenye mitaa

Hiyo ni nusu ya kwanza ya ubeti wa tatu, anaomaliza kwa kuwashangaa wanadamu kwa kuhesabu mabaya tu na kuyaacha mazuri, huku wakishangaza zaidi kwa kutangaza amani, huku wameficha mapanga viunoni mwao.

Wanahesabu mabaya tu na mema hawayaoni
Wanakuchekea machoni, wanakuroga moyoni
Wanacheka chini chini wakati una msiba
Wa kwanza kukutangaza kwa watu ukiwa na shida
Wanatamani wapangue kila Mola alichopanga
Wanatangaza amani, huku wameficha mapanga

Huyo ndie Profesa Jay, mkali ambaye kwa aina yake ya mistari katika nyimbo kama ‘Chemsha Bongo’, ‘Bongo Dar es Salaam’, ‘Jina Langu’, ‘Ndiyo Mzee’, ‘Zali la Mentali’, ‘Nikusaidieje’, ‘Hakuna Noma’, ‘Piga Makofi’, ‘Msinitenge’ na nyingine aliliza watu kwa hisia.

Katika ‘Kipi Sijasikia’, mwanamapinduzi huyo wa muziki wa kizazi kipya nchini, ameanza kwa kukumbuka namna alivyobezwa alipoacha kazi na kujitumbukiza katika muziki, kabla ya kuanza kuandamwa kwa maneno alipopata mafanikio makubwa kimuziki.

Aaah, niliacha kazi nifanye muziki, wakatabiri ‘ntalost’,
Wengine wakanishauri tuloge kuondoa mikosi,
Nakomaa na muziki ingawa jua la utosi,
Naamini wote tunapita na kamwe maiti haijioshi,
Jina langu lishatumika sana kutajirisha watu,
Nyota Ndogo alishasema; kuna watu na viatu,
Bunduki haiui watu, ila watu ndo wanaua watu,
Dunia kama jalala, tazama kwa jicho la tatu,

Profesa Jay ‘Mbeba Lawama’, ameutumia wimbo wake ‘Kipi Sijasikia’ kusisitiza umuhimu wa mtu kujiamini mwenyewe na Mungu wake, huku akiahinisha changamoto mbalimbali kubwa na ndogo alizopitia, licha ya wasiopenda maendeleo yake kupambana kumshusha.

Yalisemwa mengi demu wangu alipotoroka
Ni fundisho tosha na changamoto kwa Mwanachoka
Nimepita mengi na mitihani ya kila namna
Ndio maana me sishangai wakiniita Mbeba Lawama
Washikaji wengine feki kwenye dili hawakujui
Wanadhani kila jogoo akiwika ni asubuhi
Ridhiki hamuwezi ziba labda mtaichelewesha tuu
Mnakesha mnishushe, Mwenyezi ananipaisha
Kote mlikobana kidume ndo natusua
Mnanijua nakamua, roho za wanga zinaungua

Kiitikio kilichomliza Diamond studio

Mistari minne inakamilisha kiitikio (chorus) cha wimbo huu, lakini uzito uliomo, Profesa Jay anakiri kuwa ulimtoa machozi Diamond, aliyekiimba kwa hisia zile za ‘Nitarejea’, ‘Mbagala’ na ‘Kamwambie’.

Unayehukumu ni wewe, Mwenyezi Mungu naomba unilinde
Kwenye hii vita milele, nami nishike mkono nishinde
Unayehukumu ni wewe, Mwenyezi Mungu naomba unilinde
Kwenye hii vita milele, Mwanachoka daima nishinde

“Diamond alilia machozi wakati anafanya ‘chorus’ ya ‘Kipi Sijasikia’, kutokana na mistari yake, na ilitulazimu mimi na Prodyuza P. Funk kutumia muda wetu kumrejesha katika hali ya kawaida aendelee kuimba. Ilichelewesha mchakato kusema kweli,” anakumbuka Jay.

Jaydee, Mboni waguswa

Mtangazaji wa kipindi cha ‘Mboni Talk Show’ cha East Africa TV, Mboni Masimba na nyota wa muziki wa kizazi kipya Tanzania, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ni miongoni mwa watu walioguswa na mistari ya ‘Kipi Sijasikia’.

Akizungumza na kipindi cha ‘Sun Rise’ cha Times FM, na kisha kuandika katika ukurasa wake wa Facebook, Profesa Jay alikiri kuwa ‘Kipi Sijasikia’ umepokelewa kwa hisia na mashabiki wengi ambao wameguswa na ujumbe na kuuhusisha na kilichowatokea wao.

Jay aliandika: “Ngoma hii ya ‘Kipi Sijasikia’, walinipigia simu Mboni Masimba na Lady Jaydee, ambapo Jaydee aliniambia; “Jay, exactly umeniimbia mimi,’ Masimba naye alinambia Jembe (ananiitaga Jembe), hii ngoma sasa umeamua kuniimba kabisa.”

The Heavyweight MC aliongeza: “Na sio hao tu… hao ni watu maarufu ambao wamenipigia, lakini watu wengine wananiambia mtaani kwamba huu wimbo unawahusu kwa sababu hayo ndiyo maisha wanayoishi.”

Kilivyopokewa na mashabiki mtandaoni

Katika kipindi cha wiki mbili za kuwapo kwa kibao hiko mtandaoni, hakuna shabiki aliyekiponda zaidi ya kukimwagia sifa, wakisifu mwendelezo wa makali ya Profesa Jay aliyodumu nayo kwa zaidi ya miongo miwili sasa kwenye tasnia hiyo.

Tayari wasikilizaji zaidi ya 60,000 wameusikiliza wimbo huu na wengi kutoa ‘comments’ za kumpongeza nguli huyo, njia nyingine ya kuthibitisha mguso wa ‘Kipi Sijasikia’ kwa jamii ya wapenda muziki hasa wa kizazi kipya.

Godfrey Alfred yeye ameusikiliza na kisha kuandika: “Nice song Jay we mkali broo kaza buti achana nao kwani kipi hujasikia ha ha haaaa nouma sana. Gwala kwa ‘plutnenga’ (Diamond) kama kawa kafanya yake.”

Ian Wakaba naye ameandika: “I love it when stars compliment each other on their songs… Nyota Ndogo alishasema kuna watu na viatu… Loving it From Kenya.”

Yasini Malya yeye alisema: “Daima sintawadhuru wale wote walioniasi! Wanatangaza amani huku wameficha mapanga! Big up jay.”

Haji Abeid alisema: “Ngoma hii inanikumbusha ‘JINA LANGU’.”

Hawa Amanzi ameukariri mstari huu: “Ha ha ha wanadhani kila jogoo akiwika ni asubuhi.”

Ebenezer Latonga akasema: “Keep it up bro nakukubali ujumbe umesimama.”

Wengine walioguswa na kusema chochote ni pamoja na Yasin Kondo aliyeandika: “Imesimama wanahesabu mabaya tu mema hawayaoni, wanatangaza amani huku wameficha mapanga.”

Iddi Selemani yeye amesema: “Umedhihirisha ni kwanini unaitwa ‘Heavyweight MC, big up bro.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: