Na Mwandishi Wetu, Singida.

Dereva wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Juma Juma (52) amekutwa amekufa ndani ya chumba cha kulala wageni wakati akifanya mapenzi na mhudumu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 12:30 jioni katika nyumba hiyo ya kulala wageni iitwayo Top Life ya New Kiomboi, wilayani Iramba.

Alisema mwili wake ulikutwa ukiwa umelala pembeni mwa kitanda chumbani hapo, huku akiwa amevaa bukta na fulana.

Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha Juma aliondoka nyumbani kwake saa 6 usiku na alimuaga mpangaji wake kuwa asingechelewa kurudi, hivyo asifunge mlango.

Ilielezwa hadi saa 8 usiku Juma alionekana katika baa ya Top Life akinywa pombe na mhudumu wa gesti hiyo, Agnes Mayo (32), anayesadikiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.

Pia ilielezwa Agnes alimuaga mwenzake kuwa anakwenda kanisani Jumapili iliyopita, lakini hakurudi hadi alipoonekana akiwa na Juma wakinywa pombe kwenye baa hiyo.

Kamanda Kamwela alisema Jumatatu, mmiliki wa gesti hiyo, Omary Champeke (42) alimhoji mhudumu wa baa hiyo akimtaka aeleze aliko mwenzake, kwani hakuwa amekabidhi hesabu ya gesti na baa.

“Baada ya mmiliki kutopata majibu ya kuridhisha, aliamua kuwaachisha kazi wahudumu hao na kukubaliana na uongozi wa kijiji kuwa mhudumu huyo akabidhi kila kitu kwa niaba ya mwenzake na wakati wa makabidhiano ndipo walipokuta mwili wa Juma huku chumba kikiwa kimefungwa kwa nje na ufunguo kuachwa katika chumba cha wahudumu.

Uchunguzi wa daktari unaonyesha Juma alikufa zaidi ya siku moja toka mwili wake upatikane na haukukutwa na jereha lolote.

Hata hivyo, uchunguzi zaidi wa kipolisi unaendelea pamoja na kumtafuta mhudumu aliyetoroka, ili ahojiwe na kisha kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili endapo atabainika kuhusika na tukio hilo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: