Makachero wa FBI kutoka Marekani wamewasili nchini Tanzania kusaidia katika upelelezi wa shambulizi la bomu lililotekelezwa katika kanisa katoliki mjini Arusha siku ya jumapili.

Mwandishi wa BBC, Baruan Muhuza akiwa mjini Arusha alisema makachero hao wa FBI wako Tanzania kusaidiana na Jeshi la wananchi wa Tanzania na Polisi kutafuta undani wa tukio hili ambalo limeishtua na kuiweka serikali ya Tanzania katika wakati mgumu.

Baruan Muhuza aliongezea hali inaonekana kuwa ngumu zaidi hasa kutokana na aina ya matukio ambayo yamekuwa yakitokea katika siku za hivi karibuni yakihusisha viongozi wa dini ambapo wengi ya wanaodhurika huwa ni wa imani ya kikristo.

Wakati huo huo wakuu wa serikali wakishirikiana na viongozi wa kidini wameandaa mkutano utakaojumuisha viongozi wapatao 200.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiq amewaambia wanahabari kuwa wamelazimika kuandaa mkutano huo wa siku mbili kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete.

Mkutano huo utajadili uhusiano bora baina ya wakrito na waislamu.

Polisi nchini Tanzania inawashikilia watu wa nane kwa madai ya kuhusika na mlipuko wa siku ya jumapili katika kanisa Katoliki la Olasit viungani mwa mji wa Arusha.

Miongoni mwa washukiwa ambao wako mikononi mwa polisi ni raia wanne wa Saudi Arabia, na wengine wanne ni raia wa Tanzania.

Habari kwa hisani ya BBC Swahili.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: