Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametoa taarifa yake ya mwaka 2011/2012 na kuonyesha kuwa kuna skandali kubwa sana katika akaunti ya Deni la Taifa. Nanukuu ‘Uhakiki wa mchanganuo wa madeni ya Taifa kama ulivyokuwa tarehe 30 Juni, 2012 ulibaini kuwepo kwa marekebisho ya deni ya shilingi 619,803,554,183.91 ambayo uongozi haukuweza kutoa maelezo ya kuridhisha.’ (Taarifa ya CAG, Ripoti ya Serikali Kuu 2011/2012 uk 158). Mwisho wa Kunukuu
Katika Taarifa yake hiyo CAG anaendelea kuonyesha kuwa Deni la Taifa linazidi kukua na mwaka unaoishia mwezi Juni 2012 deni lilikuwa kwa asilimia 17 kutoka mwaka unaoishia mwezi Juni 2011.
Kukosekana kwa maelezo ya kuridhisha kuhusu zaidi ya nusu trilioni za Deni la Taifa ni jambo linalopaswa kutiliwa mashaka makubwa, kuchunguzwa na kupata majawabu stahiki. Tafiti mbalimbali duniani zinaonyesha kuwa kuna mahusiano makubwa sana kati ya Deni la Taifa la utoroshaji wa fedha kwenda kwenye mabenki ya ‘offshore’. Katika kitabu cha ‘Africa’s Odious Debts: How Foreign Loans and Capital flight bled a continent’ kilichoandikwa mabwana Leonce Ndikumana na James Boyce imeonekana kwamba Deni la Taifa huchochea utoroshwaji wa Fedha kwenda kuficha nje ya Tanzania.
Mabilioni haya kwenye akaunti ya Deni la Taifa yanashtusha sana. Kambi ya Upinzani Bungeni kwa miaka miwili mfululizo imekuwa ikitaka ukaguzi maalumu kwenye akaunti za Deni la Taifa lakini Serikali imeshindwa kufanya hivyo. Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC pia nimemtaka CAG afanye ukaguzi huu maalumu.
Kambi ya upinzani Bungeni ilisema hivi katika Bajeti yake kivuli 2012/13:
DENI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika kwa serikali kuendelea kutengeneza madeni kwa Taifa kwa kuendelea kukopa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya serikali. Wakati Serikali inasisitiza kwamba Deni letu linastahmilika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya kukua kwa Deni la Taifa. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni la Taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38% kutoka shilingi trillion 10.5 mwaka 2009/2010 hadi shilingi trillion 14.4 mwaka 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha Deni la Taifa limefikia shilingi trillion 20.3 mpaka ilipofika mwezi Machi mwaka 2012. Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia shilingi trillion 22.
Mheshimiwa Spika, Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini? Bajeti ya Mwaka 2012/13 inayopendekezwa inaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni 8.7 kama makusanyo ya ndani na itatumia shilingi trilioni 10.6 kama matumizi ya kawaida. Ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo ambayo serikali inachukua sasa itakwenda kwenye matumizi ya kawaida. Hatutaki mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari nk. Tuchukue mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi. Bajeti inaonyesha kwamba Serikali itakopa shilingi takribani trillion 5 mwaka 2012/13. Serikali ikubalikutekeleza mapendekezoya Kambi ya Upinzani ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupanua wigo wa kodi katika maeneo muhimu kama sekta ya madini na mawasiliano, kuzuia misamaha ya kodi, kutokomeza ukwepaji kodi, na kuepuka matumizi mabaya ili kuepuka madeni yasiyo ya lazima.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kusisitiza kwamba Bunge lifanye ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya Deni la Taifa ili kuweza kubaini ukweli kuhusu ustahmilivu wa Deni na mikopo ambayo Serikali inachukua kama inakwenda kwenye Maendeleo na miradi ipi na kama miradi hiyo ina tija. Vilevile tumependekeza kwamba Mikopo yote ambayo Serikali inachukua iwe inapata idhini ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi au Bunge litunge sharia ili kiwango cha juu cha kukopa ambacho Serikali haipaswi kuvuka. Kuiacha Serikali inaendelea kukopa bila mpango ni kuliweka Taifa rehani na kupeleka mzigo wa kulipa madeni haya kwa kizazi kijacho. Hatuwezi kukubali Wazee wetu waishi maisha yao, waishi maisha yetu na pia wakope maisha ya watoto wetu. Mwisho wa kunukuu.
Kambi ya Upinzani inarejea kutaka ukaguzi maalumu kuhusu akaunti za Deni la Taifa na maelezo ya kina ya Serikali kuhusu shilingi 620 bilioni ambazo hazina maelezo kwenye Deni la Taifa. Hatuwezi kukaa kimya kuona Watanzania wanabebeshwa madeni ambayo kimsingi ni madeni bandia yanayotajirisha watu wachache wenye uwezo na ujasiri mkubwa wa kuiba, kupora nakufisidi hazina ya Taifa letu.
Kabwe Zuberi Zitto,Mb
Waziri Kivuli Fedha na Uchumi
Toa Maoni Yako:
0 comments: