Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar

 Mashirikisho mawili ya Majeshi ya Polisi Barani Afrika yamekubaliana kuunganisha nguvu za pamoja katika kukabiliana na Magenge makubwa ya kihalifu wa kimataifa ukiwemo ugaidi, uharamia na biasashara haramu ya dawa za kulevya.
 
Mashirikisho yaliyofikia makubaliano hayo ni SARPCCO ya Majeshi ya Polisi kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na EARPCCO ya Majeshi ya Polisi ya nchi za Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika (EAC).
Wakitiliana saini makubaliano hayo mjini Zanzibar, Wakuu wa Mashirikisho hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema wa SARPCCO na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Rwanda Kamishna Jenerali Emmanuel Gasana wa EARPCCO, wamesema hatua hiyo ni mwanga mpya katika kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka kwa nchi za bara la Afrika.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Husein Laiser, amesema kwa muda mrefu sasa genge moja la kihalifu kutoka nchi zilizopo katika shirikisho moja hushirikiana na magenge mengine ya upande mmoja jambo ambalo amesema nivigumu kwa nchi moja kuyakabili kwa urahisi.
Amesema kwa mfano gari ama madawa ya kulevya yanaweza kusafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine na msafirishaji akaungana na kundi lingine katika nchi ya ugenini pasipo shaka ya kukamatwa kwa urahisi.
Kamanda Laiser amesema ushirikiano huo utakuwa ni daraja la kusaidia kuwakabili kwa pamoja watuhumiwa kama hao ambao wengi wao wamekuwa wakiungana na wenzao katika mataifa mbalimbali kufanikisha uhalifu wao.
Naye ACP John Bosco Kabera, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Rwanda, amesema uamuzi huo uliofikiwa utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabili matukio ya kihalifu katika ukanda huu wa nchi za Kusini na zile za maziwa Makuu.
Shirikisho la Majeshi ya Polisi kwa nchi za Maziwa makuu na Pembe ya Afrika SARPCCO, inajumuisha nchi  12 ambazo ni Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya na Tanzania, na zile zilizopo katika Pembe ya Afrika ambazo ni Sudan, Shelisheli, Ethiopia, Eritrea, , Djibouti, Sudan na Somalia.
Na Shirikisho la Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika zipo 15 zikiwemo nchi za Tanzania na Shelisheli ambazo zote zinaingia katika Mashirikisho yote mawili ya nchi za Kusini mwa Afrika na zile za Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika.
Nchi nyingine ni Angola, Afrika ya Kusini, Congo DRC, Lesotho, Msumbiji, Mauritius, Madagascar, Swaziland, Botswana, Malawi, Zambia, Zimbabwe na Namibia.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Rwanda pamoja na ujumbe wake walikaribishwa kushiriki katika mkutano wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC uliomalizika juzi mjini Zanzibar.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: