Katibu Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amewataka wahitimu na wale wote wanaopeleka maombi ya nafasi za kazi katika Sekretarieti ya Ajira kuwasilisha vyeti vyao halali na kuachana na tabia ya kutumia vyeti vya kugushi maana pindi watakapobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Daudi amesema hayo leo, ofisini kwake jijini Dar es Salaam alipokuwa akihojiwa na baadhi ya Waandishi wa habari.

Amesema ameamua kutoa tahadhari hiyo hivi sasa baada ya ofisi yake kukamilisha utaratibu madhubuti wa kuweza kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote watakaobainika kugushi vyeti katika kupeleka maombi ya kazi.

“Napenda wananchi wajue kuwa kutokana na njia tunazozitumia katika mchakato mzima tangu kutoa matangazo, kufanya usaili hadi kufikia hatua ya kuwapangia vituo vya kazi wale waliofaulu katika usaili kuwa za kisasa ni rahisi kuwabaini wale wote watakaotumia vyeti vya kugushi katika kuomba nafasi za kazi” alisema Daudi.

Aidha, amesema kuwa kazi ya kukagua vyeti vya kugushi ni ya kudumu kwa mujibu wa mfumo na taratibu zilizopo na litaendelea kufanyika kwa fani zote na ngazi zote za nafasi za kazi zinazotangazwa ili kuweza kutoa fursa za ajira kwa wale wanaostahili tu.

Amehitimisha, kwa kuwataka wale wote wanaopeleka maombi ya kazi katika Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira kuwa wakweli kwa kuwasilisha vyeti vyao halisi maana Ofisi yake haitasita kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria mtu yeyote atakayebainika kutumia vyeti vya kugushi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: