Tunaibiwa hatuimbiwi. Hicho ni kichwa cha habari nilichokiona karibuni katika gazeti moja yakiwa ni malumbano kati ya wasanii kadhaa wa filamu kwa upande mmoja na Shirikisho la Filamu Tanzania, kwa upande mwingine. Katika historia ya biashara ya sanaa katika nchi hii, si mara ya kwanza hali kama hii inatokea.

Wakati biashara ya kuanza kuuza kanda za muziki wa bendi za Tanzania inaanza, kulikuweko makundi yenye msimamo wa aina hii , walikuweko wasanii ambao walikuwa upande wa wasambazaji wa kazi za muziki wakiwatetea wasambazaji kuwa ni wakombozi wa tasnia. Wakati huo album ilikuwa ikiuzwa shilingi 30,000.

Kulikuweko na wanamuziki ambao walikuwa kama wakala wa wasambazaji wakipita kwenye bendi na kuzishawishi kuuza kazi zao, hata baadhi ya viongozi wa CHAMUDATA walishiriki kuchukua kazi za wasanii na kuiuza album nyingi za bendi kwa mfumo huo. Uchunguzi mdogo utaonyesha kama kweli hawa walikuwa wakombozi au wezi.

Kulikuweko na kundi lililopinga mtindo huu wa kuuza kazi na hilo lilionekana kama kundi linalozuia maendeleo. Mfano mwingine ni RTD iliyokuwa na bado ni moja ya wauzaji wa kanda za wanamuziki, jitihada ya kuwasaidia wanamuziki wapate fungu lao katika biashara hiyo, ilipigwa vita na baadhi ya wanamuziki waliotetea RTD kuuza kanda hizo kwa maelezo kuwa RTD imesaidia sana wanamuziki. Mpaka leo kuanzia miaka ya tisini biashara hiyo inaendelea.
Picha iliyopo kwa sasa inafanana sana na picha ya wakati huo. Kuna wasanii ambao wanauhakika wa kuuza kazi zao kwa wasambazaji na pia wanauhakika wa misaada mingi ya kuwaweka katika hali nzuri mbele ya jicho la jamii hivyo wao wanatetea hali iliyoko kuwa hawaibiwi. Upande wa pili kuna wasanii ambao wamejikuta wanashindwa kusambaza kazi zao, wala kupata mahala pa kuuza kazi zao, labda pale wanapokubali kuuza kwa ujira mdogo ambao wanaona haukidhi hata malipo ya utayarishaji wa kazi, hawa wanalalamika kuwa wanaibiwa.

Simon Mwakifwamba Rais TAFF

Katika tasnia ya filamu kuna wadau wa aina tofauti, kuna wasanii waigizaji, kuna watengeza filamu, kuna wasambazaji, baadae kuna vyombo vya urushaji wa matangazo ya filamu na video kama vile TV, DSTV na kampuni kadhaa za usambazaji kazi kwa njia ya Cable, pia wahusika wengine wengi kama watunzi wa hadithi , waandishi wa script, waongozaji wa filamu na kadhalika.

Kati yao hawa kuna  aina mbalimbali za haki. Wasanii waigizaji hulindwa na sehemu ya hakimiliki inaiyotajwa kama hakishiriki, na hawa kwa kawaida hulipwa moja kwa moja kutokana na nafasi walizoigiza katika filamu au umaarufu wao na kadhalika. Hivyo msanii anaingia makubaliano ya kulipwa aidha kwa kila scene au kwa ujumla wa  filamu nzima(Project). Hivyo kwa mtizamo huu wa mwanzo wasanii waigizaji huwa hawana cha kuibiwa kwani wanakuwa wamekwishalipwa na watengenezaji wa filamu.

Kundi la pili ni la watengezaji wa filamu ambao wao ndiyo huwa  wanajukumu la kuwalipa waongozaji, waandishi wa script, na wasanii waigizaji,na washiriki wengine katika filamu. Hawa hutegemea kupata fedha zao kutokana na malipo wanayopata kwa wasambazaji. Hapa ndipo ugomvi wa nimeibiwa sijaibiwa unapopata kelele zaidi. Watengeza filamu wanalalamika kuwa wanawekewa masharti ambayo yanadumaza tasnia ya filamu.

Baadhi ya masharti ambayo yamekuwa yakilalamikiwa ni wasambazaji kulazimisha ushiriki wa wasanii ambao wasambazaji wanaona ‘wanauza’, au hata kulazimishwa kubadili hadithi. Nilikutana na kikundi cha sanaa Iringa ambacho kilipewa masharti ya kumhusisha msanii fulani maarufu ndipo filamu yao ingesambazwa na msambazaji maarufu. Tatizo jingine ni kulazimishwa kuingia katika mikataba ambapo filamu nzima hununuliwa na msambazaji.

Mwenye filamu huwa na haki nyingi katika filamu, kurudufu, kusambaza, kutafsiri lugha, kubadili kazi(kwa mafano kutumia kipande katika matangazo), kurusha katika vyombo vya habari, kupeleka nje ya nchi nakala za kazi husika, kuingiza nchini nakala za kazi husika, na kadhalika, sasa katika kuuza haki zote hizo hukabidhiwa anaenunua, jambo ambalo linaleta utata kwani msambazaji kazi yake ni kusambaza tu. Kubwa zaidi sheria ya Hakimiliki ya nchi yetu inaeleza kuwa hakimiliki hudumu kwa maisha yote ya mwenye hakimiliki, na miaka hamsini baada ya kifo chake.

Sasa swali ni bei gani unaweza ukanunua haki zenye thamani ya umri huu? Katika nchi zenye mfumo bora wa utawala wa kazi za sanaa, msambazaji huingia makubaliano ya usambazaji kwa makubaliano yanayompa muda kamili wa usambazaji, eneo ambalo msambazaji anaruhusiwa kusambaza. Hii inampa mwenye kazi uwezo wa kubadili msambazaji pale anapoona kazi yake haisambazwi vizuri au haisambazwi kabisa.

Katika nchi hii kutokana na wasambazaji kuhodhi kazi ya usambazaji utakuta kazi zinachelewa kusambazwa na hivyo kwa wahusika kukosa mapato au la filamu yao kutoka wakati usiomwafaka na hivyo kukosa soko na kubakia kubeba kawama kuwa hawakuwa na kazi bora. Watayarishaji hujikuta filamu zao zikionyeshwa kwenye TV, au katika vyombo vingine vya kurusha matangazo bila ya wao kufaid kitu, kwani wameshauza kazi hizo. Mfanya kazi moja wa TV hapa nchini aliniambia filamu wanaletewa na wasambazaji, msambazaji haki yake ni kusambaza biashara ya kurusha matangazo huwa si yake kamwe.

Jambo baya ambalo limeingia katika tasnia hii ya filamu ni juhudi za makusudi za kuwamaliza wasambazaji wadogo. Duniani kote kuna wasambazaji wakubwa na wadogo. Mfano una mtaji wa kuweza kusambaza filamu yako, hilo ni jambo zuri , kilichofanyika katika miaka ya karibuni ni wasambazaji wakubwa kushasha bei ya ya jumla kutoka shilingi 3000 kwa nakala hadi chini ya shilingi 2000 kwa nakala hivyo kuwazuia wasambazaji wadogo kuweza kufanya kazi. Hii imelazimisha kila mtengenezaji kuwasujudia wasambaji wakubwa tu ambao ndio hutoa masharti, na kudai kuwa hawajamlazimisha mtu kuja kwao.

Taratibu ambazo zinachukuliwa na wasanii wanodai hawaibiwi ni kumwendea msambazaji na kumtajia kiasi cha fedha ambacho kitahitajika katika kutengeza filamu na hupewa kiasi hicho kadri ya makadirio yao, na filamu hiyo huwa mali ya msambazaji. Kuna taarifa za wasanii wa aina hii kuwa na mikataba ambayo hairuhusu kutengeza filamu nje ya kampuni za usambazaji, aidha wengine kupewa malipo ya gari moja kwa kutengeneza filamu hata zaidi ya tatu. Ni wazi hapa ukosefu wa uelewa wa ukubwa wa biashara hii ndio unaoleta msanii kukubali malipo duni namna hii na kuona hajaibiwa.

Jambo lililowazi ni wasanii kuchukua muda na kupata elimu kuhusu haki zao ambazo wakizielewa zitawasaidia kuishi vizuri hata pale ambapo majina yao si maarufu tena , au wasambazaji watakapoamua kuwatosa kwa jili ya kuingiza damu mpya katika biashara zao. Hakuna kitu kinachodumu milele.

Swala la Serikali ya Tanzania kutokuelewa ukubwa wa biashara hii ni tatizo kubwa sana. Katika nchi nyingine serikali huwa na mkono katika shughuli za aina hii kwani ni chanzo kikubwa sana cha pato la taifa na nafasi yenye ajira nyingi kwa wananchi

Ugomvi unaoendelea sasa katika tasnia ya filamu unatimiza usemi maarufu wa wahenga- VITA VYA  PANZI FURAHA YA KUNGURU
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: