LONDON, England

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger, ameelezea kushangazwa na uzembe uliofanywa na vijana wake na kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Bolton Wanderers juzi, ambao umefuta matumaini ya kutwaa walau taji moja msimu huu na sasa ana uhakika wanamaliza tena msimu wakitoka kapa.

Arsenal sasa imeachwa kwa pointi tisa na vinara wa ligi hiyo, Manchester United, huku zote zikiwa zimesaliwa na mechi nne kumaliza ligi, hivyo kumfanya Wenger sasa kubaki na kazi ya kupigania walau nafasi ya pili na si ubingwa.

Mshambuliaji chipukizi wa Chelsea anayekipiga kwa mkopo Bolton, Daniel Sturridge, ndiye aliyeanza kuwapa maumivu Arsenal baada ya kupiga bao katika kipindi cha kwanza na ilikuwa bahati tu kwamba Kevin Davies alikosa penalti mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Arsenal walisawazisha kwa bao la Robin van Persie na kuleta matumani ya kuondoka na ushindi kutokana na kufanya mashambulizi ya uhakika lakini bao la Tamir Cohen dakika za mwisho liliwavunja mbavu na kuhitimisha mbio zao za ubingwa.

“Ni vibaya kupoteza mechi kama hii kwa kweli, kukubali kufungwa kunamaanisha kuwaachia wenzetu kupigania ubingwa na kujiweka kando,” alisema Wenger.

Alisema wachezaji wake walichanganywa na bao la kipindi cha kwanza na wakapoteza umakini kiasi kwamba wapinzani wao walikuwa makini kiasi kwamba hawakutoa mwanya kwao kupanga mashambulizi.

Alisema kuwa nafasi pekee waliyoipoteza Arsenal msimu huu ni kukubali kufungwa na Birmingham katika Kombe la Ligi, huku ushindi huo ukiwa faraja kwa Bolton ambayo ilichapwa mabao 5-0 na Stoke City na kung’olewa katika nusu fainali ya Kombe la FA.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: