*NI YA VIJANA CHINI YA UMRI WA MIAKA 16
*YASHIRIKISHA SHULE 6 ZA KINONDONI
*WAZAZI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI
Na Mwandishi wetu
Mashindano ya mchezo wa soka ya DAR SECONDARY SCHOOL CUP yanayoshirikisha vijana wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam wenye umri chini ya miaka 16 yamezinduliwa rasmi katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar – UDSM.
Mashindano hayo yameandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Upendo Youth Development Organization – UYODEO lenye makao yake makuu huko Kilwa – Masoko.
Akizungumza na MO BLOG Mjumbe wa Heshima wa UYODEO na Mratibu wa mashindano hayo Annick Verstraelen amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kuwakutanisha pamoja wanafunzi kutoka shule mbali mbali chini ya kauli mbiu ya ‘TUCHEZE PAMOJA’ ili waweze kufahamiana, kushiriki michezo pamoja na kujenga uhusiano.
Amefafanua kuwa mashindano hayo pia yanalenga kutafuta, kukuza na kuvitumia vipaji miongoni mwa wanafunzi ili waweze kujitambua wakiwa bado katika umri wa kukua.
Mashindano hayo mwaka huu yamehusisha timu za shule sita (6) kutoka wilaya ya Kinondoni, lakini ni matarajio ya UYODEO kupanua wigo ya mashindano hayo na kufanyika pia katika wilaya za Ilala na Temeke.
Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo katika kuandaa na kufanikisha mashindano hayo, Annick amesema uhaba wa fedha umekuwa ni kikwazo kikubwa kutokana na gharama za maandalizi kuwa kubwa ikilinganishwa na uwezo wa shirika hilo, hivyo ametoa wito kwa wadhamini kujitokeza ili kuwezesha mashindano hayo kufanikiwa kwa kiwango kilichokusudiwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: