Uamuzi huo umetangazwa jana kwa nyakati tofauti na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wali.
Shirima amewaambia waandishi wa habari mjini Arusha kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na utaratibu aliojiwekea mchungaji huyo kwamba hatatoa tiba siku za Ijumaa Kuu na Jumapili ya Pasaka. Mbali na kusitishwa kwa safari hizo kwa muda, watu wanapaswa kuzingatia utaratibu wa kwenda Samunge kwa vibali ili kuondoa msongamano usiokuwa wa lazima.
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapila ameiomba Serikali idhibiti uingiaji zaidi wa magari yanayopeleka wagonjwa kupata tiba katika Kijiji cha Samunge kutokana na foleni kuwa kubwa na kutishia maisha ya wagonjwa.
Akizungumza kwa niaba ya mchungaji huyo, Msaidizi wake, Fred Nsajile amesema kama magari yasipodhibitiwa hasa yanayotoka Kanda ya Ziwa, vifo vinaweza kutokea.
60 WANUSURIKA AJALINI WAKIELEKEA KWA BABU.
Zaidi ya watu 60 wamenusurika kufa jana alfajiri baada ya basi walilokuwa wamepanda kutoka Kondoa, mkoani Dodoma kuanguka kabla ya kufika Samunge.
Basi hilo lililokuwa linaendeshwa na Idrisa Ramadhani lilianguka majira ya saa 10 alfajiri likiwa linashuka katika mlima uliopo eneo la Mdito. Baadhi ya abiria ambao wamejeruhiwa wamelazwa katika kituo cha afya cha Samunge na hakuna aliyefariki.
WAGENI WAZIDI KUONGEZEKA SEMUNGE.
Raia wa nchini Uganda jana walianza kuingia kwa wingi Samunge, sambamba na wale wa Kenya ambao hadi jana mchana walikuwa wamefikia 2,568.
Raia wengine waliokwishafika Samunge ni wa nchi za Lebanon, Sweden, Uingereza, Zimbabwe, Rwanda, Uholanzi na Falme za Kiarabu (UAE).
Toa Maoni Yako:
0 comments: