Pichani ni waandishi wa habari wakiwa kazini.
----
Siwezi kukaa kimya kuhusu mjadala huu. Matatizo yapo tena makubwa sana katika sekta ya habari kwa maana ya wanataaluma wenyewe. Lakini mtazamo wangu ni kwamba;
1. Hatuwezi kuondokana na matatizo haya kwa kulaumiana. Lawama huwa haziondoi matatizo, lazima mifumo iliyopo ichukue hatua stahili za muda mfupi na za muda mrefu kukabiliana na kawalaumu hatuwezi kuondokana na matatizo yaliyopo.
2. Lazima tufahamu kwamba mfumo wa nchi yetu wa uendeshaji wa mambo bado una ujima ndani yake. Tukiacha vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali, lakini vipo vyombo vya habari vingine ambavyo vimeanzishwa kwa malengo ya kulinda maslahi ya hao walioko serikalini. Sera zake zimetungwa ili kukidhi matakwa ya waliovianzisha. Sasa hapo tutawalaumu waandishi wa habari ndiyo, lakini ukweli ni kwamba wakati wakiingia katika vyombo hivyo walijua kabisa kwamba wao ni 'guard dogs'.
3. Waandishi wa habari ni wanadamu kama walivyo wengine. Hivyo basikatika kundi lao wapo ambao wanautumikia umma wa Watanzania. Wapo wenye uwezo wa kuhimili mikikimikiki na dhoruba kutoka pande zote (kwa wanasiasa, wafanyabiashara, mafisadi na wengine wengi). Lakini wapo ambao hunywea kila wanapodhani kwamba maisha yao yako hatarini kutokana na jinsi wanavyotekeleza wajibu wao. Hivyo basi si ajabu kuwa na makundi hata kumi yenye tabia tofauti katika fani ya waandishi wa habari. Ni vigumu kuwa na 'akina Mgamba wote' katika fani hii.
4. Mimi naamini kwamba uhuru wa mwandishi wa habari unaanza na yeye mwenyewe. Anajiamini kiasi gani, ni mwaminifu kiasi gani katika dhamira yake na zaidi ya yote anawezaji kutekeleza bila woga yale anayotumwa na dhamira yake. Hapa ndipo tofauti zinapotokea maana dhamira huwa haiongopi. Wapo wanaoamua kwa makusudi, au kwa kupewa fedha au kwa kuahidiwa cheo (kuwa dc, rc nk.) kusaliti dhamira zao wenyewe. Wakaukana ukweli na kuwa waumini wa uwongo. Hili lipo na si katika sekta ya habari pekee hata kwa Maaskofu na Mashehe.
5. Ninachojaribu kuieleza ni kwamba ili kuwa na sekta ya habari imara pengine kuliko tuliyonayo sasa, mchakato ni mkubwa na tunaanza na maadili ya mwandishi wa habari mmoja mmoja na baadaye katika ngazi nyingine. Ila kulaumiana hakuwezi kusaidia lazima hatua tuzichukue. Sisi ndani ya Jukwaa la Wahariri tumeanza na wengine tufuate nyayo.
Neville C. Meena,
Secretary General,
Tanzania Editors' Forum (TEF),
Dar es Salaam -Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments: