Naam! Hizi ndio kauli za wabunge wetu wakiwa bungeni wanataka ahadi za rais zitekelezwe majimboni mwao , wamelaza bongo zao hawataki kufikiri wanangoja ahadi za rais zitekelezwe huku mawaziri nao wakichombeza na kuitikia wimbo huohuo wa utekelezaji wa ahadi za rais..aibu tupu!
Inasikitisha kuona kuwa badala ya mbunge kubuni na kuja na mikakati ya maendeleo kwa kuwashirikisha wananchi wake yeye anaenda bungeni kulialia ili ahadi za rais zitekelezwe ndiyo ni kulialia huko , huku baadhi yao wakiongea kwa mnato, madaha na mbwembwe za madaraka na cheo wanadhani sisi tunafurahishwa na tabia yao hii ya kumlilia rais au kuimba wimbo wa ahadi za rais?
Na hii ndio sababu nitaendelea kusisitiza ni bora kutokuwa na wabunge kabisa kuliko kuwa na wabunge wanaolilia ahadi za rais kwa maana hawafai hata kidogo na bahati mbaya ni kuwa hata hizo wanazoita ahadi za rais haziwezi kutekelezwa kwa maana aliahidi nyingi na hazikumbuki hivyo hawezi kuzitekeleza, haya ndiyo mambo ya viongozi wetu kuahidi fly-overs (barabara za juu) halafu hata za chini za kawaida zimewashinda nab ado hawaoni aibu wala kusikia kichefuchefu kupita kwenye barabara zilizoachwa na mkoloni, halafu useme viongozi wa namna hii wanaweza kusimamia maendeleo ya nchi?
Inauma sana tena inatia uchungu kuona kuwa mpaka leo watu wanapata tabu kwasababu ya msongamano wa magari jijini Dar es salaam, magari yanajaa mpaka watu hawapumui, inauma kuona kuwa wanafunzi wananyanyaswa na makonda utadhani ni wakimbizi kwenye nchi hii halafu mbunge anaenda bungeni kulilia ahadi za rais..alaaniwe!
Mawaziri nao wanatushangaza na tabia yao tena inakera sana ya kuogelea kwenye ahadi za rais kutekeleza majukumu yao badala ya mikakati ya wizara, labda watwambie kama wameshindwa kazi ya kusimamia na kupanga kwenye wizara zao na kuamua kutekeleza ahadi za rais basi waachie ngazi kisha tumpe huyo rais aongoze wizara zote tuone kama ataweza? Kwa maana masikio yetu yamechoshwa na neon rais sasa tumechoka tunataka kusikia neno maendeleo.
Naam! ni bora kutokuwa na mawaziri na wabunge kuliko kuwa na mawaziri na wabunge wanaogambania na kupigana vikumbo kutekeleza ahadi za rais na heri mara mia kuwa na taifa lililo jangwani lakini linaongozwa na mikakati na mipango ya maaendeleo kwa kushirikisha wananchi wote kuliko kuwa na taifa lenye utajiri mkubwa na maliasili zisizohesabika kama Tanzania halafu linaongozwa na ahadi za rais.. Tafakari!
Kitendawili si deni ukishindwa nipe mji, Kwa wanataaluma kutofautiana kimawazo si kosa bali ni dalili ya jamii iliyo hai, Nova Kambota Mwanaharakati,
Nipigie; 0717-709618 (Tanzania)
+255717-709618 (Nje ya Tanzania)
Niandikie; novakambota@gmail.com
Nitembelee; www.novatzdream.blogspot.com
Tanzania, East Africa,
Jumamosi 16 April, 2011.
Toa Maoni Yako:
0 comments: