WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema zao la zabibu halina budi kutiliwa mkazo kwa sababu lina fursa kubwa ya kukuza uchumi wa wananchi wa mikoa ya kati kwa vile linavunwa mara mbili kwa mwaka.

Ametoa kauli hiyo juzi usiku (Jumamosi, Aprili 16, 2011), wakati akizungumza na wabunge na wafanyakazi wa ofisi ya Bunge katika tafrija fupi iliyoandaliwa na kampuni ya Tanzania Distilleries Limited (TDL) ili kuelezea kampuni hiyo inafanya nini mkoani Dodoma.

“Nimefarijika kuelezwa kuwa soko la zabibu siyo tatizo tena... inabidi tuishawishi na mikao jirani ya Singida ambako hali ya hewa ni kama hapa Dodoma ili nao walime zao hili,” alisema.

“Niliwahi kwenda kwenye shamba la Mzee Kusila (William), nilishangaa jinsi alivyoamua kujikita katika zao hili, nilipomuuliza anapata kiasi gani, alinijibu kuwa akikosa sana ni kama sh. milioni 30,” aliongeza.

Waziri Mkuu alisema zao la zabibu zaidi ya kilimo, lina fursa pia ya ufugaji nyuki kwani naye anatumia eneo lake kuweka mizinga. “Mimi nalima zabibu za mezani (siyo za mvinyo), lakini maua ya zabibu ni kichocheo kizuri cha asali kwani nyuki wanapata chavua kutoka pale... kwa hiyo huku ninalima zabibu lakini pia napata asali,” alisema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu azungumze na wabunge, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bibi Anna Makinda alisema kampuni ya TDL imetoa changamoto kwa wabunge wa mkoa wa Dodoma kuhimiza zao la zabibu kwa wananchi wao.

“Hii ni fursa ya kipekee, nawasihi Wabunge wa mkoa wa Dodoma waunde umoja wao, wawahimize wakulima kulima zaidi zabibu kwa sababu TDL wapo... ninyi kama wabunge hamna kitu kizuri cha kuwapa wakazi wenu zaidi ya hiki,” alisema.

“Wenzenu wa mikoa ya Kusini kila siku utawasikia wanawatetea wakulima wao kuhusu zao la korosho, nanyi pia wateteeni wa kwenu kuhusiana na zao la zabibu ili waweze kubadili maisha yao,” alisisitiza.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya TDL, Bw. Alex Samamba aliwaeleza wabunge waliojumuika katika tafrija hiyo kwamba katika miaka minne iliyopita, kwa kupitia wakulima wa zabibu ambao wameingia nao mkataba, wameweza kuinua kiwango cha uzalishaji kutoka tani tatu hadi tani nane kwa mwaka.

Alisema hadi sasa wamekwishawafundisha wakulima wasiopungua 50 kuhusu mbinu za kilimo bora cha zabibu ambao wanatoka vijiji vitano vya Makang’wa, Hombolo, Mpunguzi, Kibelela na Mbabala vilivyoko katika wilaya za Kongwa na Dodoma mjini.

“Zabibu za Dodoma zinavunwa mara mbili kwa mwaka wakati katika nchi nyingine huwa inavunwa mara moja tu kwa mwaka, alisema na kuongeza kwamba umefika wakati sasa Watanzania hawana budi kuupenda mvinyo unaotengenezwa hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo watawawezesha wakulima wa zabibu kuongeza kipato,” alisema Bw. Samamba.

“Ninawaomba ndugu zangu muuthamini mvinyo wa Tanzania, muuthamini utanzania wetu kwani sasa hivi tunatengeneza mvinyo aina ya Overmeers katika viwango vya kimataifa. Unaponunua mvinyo huu utamsaidia mkulima aweze kusomesha watoto wake,” alisema.

Alisema mbali ya Overmeers, kampuni hiyo inatengeneza mvinyo aina ya Dodoma na Imagi pamoja na pombe kali (brandy) aina ya Valeur kutokana na uji wa zabibu za Dodoma.

(mwisho)

OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, APRILI 17, 2011

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: