Mkongwe wa Hip Hop nchini Profesa Jay anatarajia kupanda jukwaa moja na kundi la muziki wa dansi la Mapacha Watatu Jumapili ya Pasaka.
Mmoja wa wanamuziki wa kundi hilo, Khalid Chuma ‘Chokoraa’, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, onyesho hilo la aina yake, litafanyika ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama, jijini.
“Tutakuwa na MC Shupavu katika show ambayo itakuwa tofauti kabisa na zingine tulizowahi kufanya. Hii itakuwa ni zawadi rasmi kwa mashabiki wetu ambao wametuunga mkono kwa kipindi chote,” alisema Chokoraa.
Mwimbaji huyo alisema siku hiyo pia kundi lao litatambulisha kibao chao kipya kilichotungwa na Erasto Mashine unaoitwa ‘Gari Bovu’.
Pia katika kunogesha onyesho hilo, mwanamuziki huyo nyota alisema wapendanao wawili watakaokuwa wamependeza kupita wengine, nao wameandaliwa zawadi maalumu siku hiyo.
Wanamuziki wengine wanaounda safu ya Mapacha Watatu ni pamoja na Kalala Junior na Jose Mara ambaye pia anafanya kazi na kundi la FM Academia.
Aidha, Chokoraa alisema siku hiyo pia ‘Babu wa Loliondo’ atakuwepo ukumbini kwa ajili ya kugawa kikombe kwa mashabiki wao.
“Tuna shabiki yetu mmoja anajiita Babu wa Loliondo, ana kawaida ya kugawa kikombe kwa mashabiki, kwa hiyo watu waje kwa ajili ya kukipata kikombe hiki,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Jay, mmoja wa waasisi wa Bongo Fleva, atapiga nyimbo zake zote zilizowahi kutamba, tokea akitamba na kundi la Hard Blastaz Crew.
Baadhi ya nyimbo atakazopiga ni pamoja na Chemsha Bongo, Zali la Mentali, Jina langu, Niamini, Nikusaidieje na nyinginezo nyingi.
Bonyeza hapo chini kusikiliza nyimbo ya Niamini kutoka kwa Hard Blastaz ambalo ndani yake alikuwepo Profesar Jay.
Toa Maoni Yako:
0 comments: