RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume leo ameungana na viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali, wananchi na wanafamilia katika mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Marehemu mzee Foum Mati huko Kandwi Kilimani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa za CCM zilizotolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Salehe Ramadhan Ferouz zilieleza kuwa marehemu mzee Foum Mati alifariki dunia jana huko nyumbani kwake Kandwi Kilimani baada ya kuugua maradhi ya moyo kwa muda mrefu.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria katika mazishi hayo ni Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Mhe. Ali Juma Shamuhuna, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Ferouz na viongozi wengine.

Marehemu mzee Foum Mati alizaliwa katika kijiji cha Jombo Matemwe mnamo mwaka 1938 na kupata elimu ya Quran kijiji kwao Jombo.

Marehemu Foum Mati katika uhai wake amewahi kuwa Mwenyekiti wa ASP Tawi la Matemwe, amekuwa mfanyakazi wa serikali akiwa Afisa Usalama wa Taifa na kuwa Mwenyekiti wa ASP Jimbo la Kaskazini A, Unguja.

Aidha, marehemu Foum aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM hadi mwaka 2007.

Marehemu mzee Foum Mati amefariki akiwa na umri wa miaka 71 na ameacha vizuka 2, watoto 15 na wajukuu 55, Mungu aiweke roho ya marehemu peponi Amin.

Habari kwa hisani ya Rajab Mkasaba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: