Articles by "ELIMU."
Showing posts with label ELIMU.. Show all posts
Dar es Salaam. Tarehe 7 Januari 2025: Katika kuukaribisha mwaka mpya 2025, Benki ya CRDB imezindua mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote. Mikopo hiyo inayoitwa Ada Fasta ni mwendelezo wa juhudi za Benki ya CRDB kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kifedha wanakokabiliana nazo.


Akizindua mikopo hiyo inayotolewa kupitia Programu ya SimBanking, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema kila mzazi au mlezi mwenye uhitaji anaweza kupata mkopo huo ili kumruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo kulingana na ratiba ya muhula husika.

“Mteja anaweza kukopa mpaka shilingi milioni 3 ambazo atazirudisha ndani ya miezi sita. Riba ya mkopo huu ni asilimia 13 tu mwaka, gharama ndogo zaidi ukilinganisha riba iliyopo sokoni. Nawakaribisha wazazi wote kuitumia fursa hii kuhakikisha watoto wetu wanasoma bila tatizo lolote la ada,” amesema Nshekanabo.

Mkurugenzi huyo amesema wameizindua huduma hiyo kipindi hiki wakitambua kuwa Januari ni mwezi wenye changamoto nyingi za kifedha zinazotokana na mahitaji makubwa yanayokuwepo ikiwamo ada za wanafunzi, kodi ya nyumba na mahitaji mengine muhimu hasa baada ya kila mtu kuwa ametumia kiasi kikubwa cha fedha kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.


Ikiwa Benki inayomsikiliza mteja na kumweka mbele katika mikakati ya biashara, amesema wakati wote wanabuni huduma na bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wateja na Januari hii wamekuja na jambo jipya mahususi kwa kila mzazi au mlezi wa mwanafunzi nchini.
Zaidi ya muongo mmoja Benki ya CRDB ilizindua nakuutambulisha Mfumo wa Makusanyo ya Ada Shuleni yaani School Fees Management System ambao mpaka sasa unatumiwa na zaidi ya shule 1,000 nchini kote ambazo sasa wanafunzi wake watanufaika na mikopo hii iliyozinduliwa.


“Hii ni fursa kwa shule zote binafsi nchini kujiunga na mfumo huu wa makusanyo ya ada ii kutoa fursa kwa wazazi kukopa ada wakati wowote watakapohitaji ili watoto waendelee na masomo yao. Wazazi wote waliopo kwenye shule zinazoutumia mfumo huu wawe ni wateja wetu ama la, wanayo fursa ya kunufaika na mikopo hii,” amesema Nshekanabo.

Mzazi au mlezi atakayeomba mkopo huu, amesema atapata fedha husika zitakazoingizwa kwenye akaunti ya shule moja kwa moja na yeye kupata risiti ya uthibitisho kwamba amelipa ada inayotakiwa kwa ajili ya mtoto wake.

Kwa kuwawezesha wazazi na walezi kulipa ada kwa wakati, Nshekanabo amesema wana imani watakuwa wamesaidia kuboresha elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo yao bila vikwazo huku shule zikiweza kujiendesha na kutoa maarifa bora yanayohitajika kwa watoto wa Kitanzania.

Kwa mzazi au mlezi ambaye ameajiriwa na mshahara wake unapitia Benki ya CRDB, anaweza kupata mkopo wa ada kwa kuingia kwenye Programu ya SimBanking kisha akabofya sehemu ya mikopo ambako atatakiwa kuingiza ‘control number’ aliyotumiwa na shule kwa ajili ya malipo ya ada na programu itamwonyesha kiasi cha juu anachoruhusiwa kukopa.
Baada ya hapo, mteja atatakiwa kuingiza kiasi anachokitaka na kupendekeza muda anaotaka kulipa deni hilo ndani ya miezi sita ili kukamilisha maombi yake. Akishafanya hivyo, Benki ya CRDB itaingiza fedha zilizoombwa kwenye akaunti ya shule anakosoma mtoto hivyo kumruhusu asome kwa utulivu.

Ukiacha faida zilizopo kwa pande zote mbili yaani shule na mzazi au mlezi, mfumo wa makusanyo ya ada wa Benki ya CRDB ni rahisi kuutumia kwani mteja anaweza kulipa ada kupitia SimBanking, CRDB Wakala au kutembelea tawi la Benki ya CRDB.

Vilevile, mteja anaweza kulipa ada ya mwanafunzi kupitia M-pesa, Tigopesa, Airtel Money au Halopesa bila kulazimika kupeleka risiti ya malipo shuleni kwani taarifa huwa zinafika huko moja kwa moja. Kwa upande wa shule, faida iliyopo ni kwamba inakusanya ada kwa wakati na kupata taarifa papo hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote (Ada Loan) iliyozinduliwa na Benki ya CRDB ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kwa kuwawezesha mkopo ili kukabiliana na changamoto za kifedha hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka. Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye ukumbi wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo.

Rais wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu nchini (TAPIE), Mahmod Mringo akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote (Ada Loan) iliyozinduliwa na Benki ya CRDB ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kwa kuwawezesha mkopo ili kukabiliana na changamoto za kifedha hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka. Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye ukumbi wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo.


MENEJA wa Wakala wa Vipimo (WMA) Phanuel Matiko, akizungumza na waandishi wa habari katika banda la WMA kwenye maonesho ya wakulima kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Na Okuly Julius - DODOMA.

MENEJA wa Wakala wa Vipimo (WMA) Phanuel Matiko amesema ili wakulima kuepuka kipimo cha lumbesa wanatakiwa kuacha tabia ya kuuzia mazao yao Shambani.

Matiko ameyasema hayo leo Agosti 7, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya wakulima kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema kuwa ili wakulima kuepuka kipimo cha lumbesa wanapaswa kuacha tabia ya uuzaji wa mazao yao ya kilimo shambani.

"Wito wangu niwaombe wakulima kuacha tabia ya kuuza mazao yao shambani ili kuepuka lumbesa bali watumie mizani kwa kuuza mazao yao kwa kilo.

"Wakulima hawapaswi kuuza mazao yao kwa kutumia debe au kisado au vitu vingine vinavyofanana na hicho bali watumie mizani ili kuepuka lumbesa kwenye uuzaji wa mazao yao,"amesema.

Amesema pia wao ni wadau wakubwa kutokana na jukumu lao la kupima usahihi wa mizani, mita za maji, umeme pamoja na pampu za mafuta.

"Moja ya majukumu yetu ni kupima usahihi wa mizani ili kile ambacho mtu atanunua kiwe kweli kinalingana na fedha yake lakini pia hivi sasa tunapima mita za umeme na maji.

"Tunakagua alichokitumia na kulipa kama ni sawa. Pia kwenye ukaguzi wa Pampu za mafuta tunakagua kiasi cha mafuta hivyo hata mkulima akipeleka trekta kujaza mafuta basi asiibiwe iwe kwenye ujazo sahihi,"amesema.

Hata hivyo amewahamasisha wakulima pamoja na wananchi kutembelea banda la WMA ili kupatiwa elimu mbalimbali inayohusu majukumu yao katika Wakala huo.

Baba Askofu Dkt Stanley Hotay wa Kanisa la Anglican akizungumza na Vijana katika kongamano la siku moja likiloandaliwa na Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya (Vuka Initiative) ambalo limebeba jina la Mlinde Mtoto wa Kiume dhidi ya Ukatili wa Ulawiti. (Picha zote na Cathbert Kajuna- Kajunason Blog/MMG.
Mkurugenzi wa Taasisi  isiyo ya Kiserikali (Vuka Initiative) Bi. Veronica Ignatus katika kongamano la siku moja lililobeba Jina la "Mlinde Mtoto wa Kiume dhidi ya Ukatili wa Ulawiti,".
Mkuu wa Dawati la Jinsia Kutoka Jeshi la Polisi SP Happiness Temu alisema "vijana wa Kiume hata kukiwepo na Shauri hata wakiitwa polisi   wanadhana potofu kuwa Dawati linawahusu wanawake tu jambo ambalo siyo kweli kwani hata wao linawahusu",.
Habiba Madebe Mratibu wa Jinsia na Malezi ya Mtoto Kutoka Arusha Jiji
Dkt. Na mtaalam wa Afya ya Akili akizungumza katika kongamano likiloandaliwa na Vuka initiative katika Chuo cha Ufundi Arusha.

Baadhi ya washiriki wa kongamano la Mlinde Mtoto wa kiume dhidi ya ukatili wa ULAWITI lililojumuisha vijana wa kiume na baadhi ya wazazi katika chuo cha Ufundi Arusha (ATC) 
Baadhi ya washiriki wa kongamano la Mlinde Mtoto wa kiume dhidi ya ukatili wa ULAWITI lililojumuisha vijana wa kiume na baadhi ya wazazi katika chuo cha Ufundi Arusha (ATC) .

Na Mwandishi wetu, Arusha

Jamii yaaswa kuungana kwa pamoja katika mapambano ya kumlinda mtoto wa kiume dhidi ya ukatili wa Ulawiti.
Hayo amezungumzwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya isiyo ya Kiserikali (Vuka Initiative) Bi. Veronica Ignatus katika kongamano lililoanyika mwishoni mwa mwezi uliopita jijini Arusha lililobeba "Mlinde Mtoto wa Kiume dhidi ya Ukatili wa Ulawiti" na kutanisha vijana wa kike na kiume wa Chuo cha ufundi Arusha (ATC) zaidi ya 100 pamoja na wazazi.

Kampeni hiyo imekuja kutoka na mmomonyoko wa maadili katika jamii na wazazi kukosa muda wa kukaa watoto wao.

Amesema kuwa watoto wengi wa kiume wamekuwa wakitendewa ukatili hata baadhi yao wamekuwa wakitishiwa jambo ambalo limewafaya kukosa ujasiri wa kujieleza, huku wengi wao wamejikuta na kauli zisizokuwa na matumaini yeyote kwao, bila kusahau sehemu kubwa ya ukatili ukiwa unafanyika nyumbani.

Bi. Veronica amesema kwamba lengo kuu la kongamano hilo ni kuwakumbusha Wazazi na Walezi kutambua umuhimu wao katika malezi na makuzi stahiki kwa watoto wa Kiume, kutambua changamoto za Ukatili wanazozipitia, sambamba na kuzitolea taarifa sehemu husika ili kuhakikisha watoto hao wanakuwa salama na kupatiwa maadili mema ili aweze kuja kuzisimamia vyema familia yake.

"Tumekuwa tukisikia/kuona baadhi ya watoto wetu wakijihusisha na mapenzi ya jinsia moja na hii ni hali inayosikitisha, Mtoto wa kiume akishaharibiwa hawezi kusaidiwa tena, tunaomba wazazi walezi viongozi mbalimbali tutupie suala hili macho kwa karibu kuwanusuru kwaajili ya familia na Taifa kwa ujumla.

Ameongeza jambo lingine linalowafanya watoto wa kiume kujiona wanyonge katika jamii ni Wazazi wamekua wakitumia muda mwingi kutafuta mali na kushindwa kumsikiliza hivyo kupelekea kumnyima haki yake ya kumsikiliza, ukizingatia ukuaji wa Sayansi na Teknolojia pamoja na muungiliano wa mila na desturi hivyo baadhi ya wazazi wanakua wakali kupita kiasi lakini pia kuna wazazi wanaowaachia watoto kila wanachokitaka hivyo kuwafanya watoto kubweteka mwishowe wanapokuwa watu wazima wanataka vitu kwa urahisi hatimaye anajiingiza kwenye vitu visivyofaa.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika kongamano hilo Baba Askofu Dkt. Stanley Hotay wa Kanisa Anglican amesema mtoto wa Kiume amekuwa akikataliwa katika Jamii, familia, shuleni hali inayompelekea kuchanganyikiwa na kutokufahamu asimame upande upi kwani amewekwa kuwa daraja la pili, hata wakati mwingine ameshindwa kufanya maamuzi ya busara kwasababu ya kukosa ujasiri.

Amesema ili vijana hao waweze kuepukana kutokana na janga lililopo la ushoga amewaomba viongozi wa dini mbalimbali, Wazazi walezi viongozi kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa kuungana kwa pamoja kutafuta mbinu mbadala ya kuwanusuru watoto wa Kiume katika changamoto iliyopo kwa sasa ili kupata Taifa Bora.

Kwa upande wake mkuu wa Dawati la Jinsia kutika Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha SP Happiness Temu amesema kuwa vijana wa Kiume hata kukiwepo na Shauri hata wakiitwa polisi hawaendi kwasababu wanachukulia kwamba Dawati linawahusu wanawake na siyo wao.

"Hii inatokana na mazingira aliyolelewa, Mila na desturi ambazo zinamuonyesha mtoto wa Kiume hapaswi kusema pale anapRoumizwa, kupigwa au kufanyiwa ukatili wa kulawitiwa ama kubakwa , kwamba italeta aibu katika Jamii yao jambo ambalo siyo sawa,kwani Mtu yeyote ana haki ya kusema pale anapotendewa ukatili wa aina yeyote.

Aidha kongamano hilo limebeba ujumbe usemao mimi ni chimbuko la Familia,Mimi ni Kichwa cha Familia Mimi ni Kiongozi ajaye ,Nilinde nisilawitiwe ,huku kaulimbiu ikiwa ni Jenga msingi bira kwa mtoto wa Kiume kwa manufaa ya Taifa Lijalo.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga (watatu kulia) akipokea sehemu ya msaada wa magodoro, viti na meza kutoka kwa Meneja wa Benki Uhusiano wa Benki ya CRDB Kanda ya Nyada za Juu Kusini, Pascalia Bura, (katikati) kwa ajili ya Shule ya Msingi ya Majimoto (Shule Maalum), katika hafla ya makabidhiano hayo, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Wilayani ya Mpimbwe, mkoani Katavi. Wapili kulia ni Mbunge wa Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Geophrey Pinda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe, Shamimu Mwariko (watatu kushoto) pamoja na viongozi wengine mbalimbali.
======== ======== ========
Benki ya CRDB kupitia sera yake ya kurudisha kwa jamii sehemu ya asilimia moja ya faida yake, imeweza kutoa msaada wa magodoro 68 pamoja na viti 24 na meza 2 kwa matumizi ya wanafunzi wenye changamoto za usikivu na madawati 25 kwa ajili ya wanafunzi wenye changamoto ya uoni hafifu na viungo katika Shule ya Msingi ya Majimoto (Shule Maalum) , iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.

Akipokea msada huo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele anayesimamia pia Wilaya ya Mpimbwe, Majid Mwanga ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuona umuhimu wa kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutatua changamoto mbalimbali za elimu hapa nchini. Ameishuru Benki ya CRDB kwa msaada huo wa magodoro, viti pamoja na meza.

Msaada huo ni muendelezo wa programu maalumu ya benki hiyo iitwayo 'Keti Jifunze' yenye lengo la kuwawezesha wanafunzi kujifunza wakiwa wameketi katika mazingira mazuri na salama. Shule Maalum ni zile zinazohudumia wanafunzi wenye changamoto mbalimbali kama vile uoni, usikivu na viungo.

Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga (watatu kushoto), Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Geophrey Pinda (watatu kushoto), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe, Shamimu Mwariko (wapili kulia), Meneja wa Benki Uhusiano wa Benki ya CRDB Kanda ya Nyada za Juu Kusini, Pascalia Bura (wapili kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Benki ya CRDB na Halmashari wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wanafunzi Shule ya Msingi ya Majimoto (Shule Maalum) iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.

Meneja wa Benki Uhusiano wa Benki ya CRDB Kanda ya Nyada za Juu Kusini, Pascalia Bura (watatu kushoto) akizungumza jambo wakati wa hafla ya kukabidhi magodoro, viti na meza


Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga akizungumza katika hafla hiyo.





Na Oscar Assenga,Tanga

CHUO cha Baharia Jijini Dar es Salaam(DMI) kimeshiriki maonyesho ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu Jijini Tanga huku wakijivunia kutoa wataalamu wenye uwezo mkubwa wa kusanifu na kuzikarabati meli kupitia Temesa na hivy
o kuondoa uhaba uliokuwepo awali nchini .

Akizungumza leo na waandishi wa habari katika Banda lao lililopo eneo la Shule ya Sekondari Popatlaly kunakofanyika maadhimisho ya elimu, ujuzi na ubunifu Captain Mohamed Kauli alisema wameshirika kwa lengo la kueleza wanachokifanya ikiwemo ufanisi wa meli,usafirisha majini, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi baharini, usanifu ini na ujenzi wa meli na ubaharia.

Alisema awali chuo hicho kilikuwa kinazalisha mabaharia wakati kilipoanzishwa lakini ili kukabiliana na ombwe la ukosefu wa ajira kutokana na vijana wengi kumaliza vyuo na kukosa ajira na wahitimu hao wanafaida kubwa mbili wanapohitimu chuo kupata ajiri nchini kwenye sekta ya usafirishaji majini na nje ya nchi kwenye meli.

“Kwa kweli tumekuwa tukizalisha idadi kubwa ya mabaharini wanaofanya kazi nje na ndani ya nchi kuna gepu kwenye utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi baharini lakini pia gepu la upatikanaji wa meli awali zimekuwa zikiagizwa kutoka nje kwa gharama kubwa”Alisema

Alisema lakini sasa Serikali imetengeza wataalamu wanaotoka kwenye chuo hicho ambao wanajenga meli,kuzisanifu ,kuzikarabati kwenye eneo hilo serikali kupitia Temesa wanajenga na kukabarati meli hizo hapa hapa nchini.

Awali akizungumza mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho, Masaka Julias alisema kwamba mafunzo ambayo wanayapata kwenye yamewawezesha kubuni vitu mbalimbali a hivyo kuwawezesha wanapomaliza kuweza kujiajiri kupitia ujuzi walioupata.

Alisema kwamba kwa sasa kupitia mafunzo hayo unawasaidia kutengeneza vitu mbalimbali vya ubunifu huku akieleza wamebuni wazo la kutengeneza mashine ya kutengeneza chilsource na ya kufunga vifuniko kwenye chupa ambayo inasahisisha.
Mratibu wa mafunzo (Supervisor Learning and Development wa Barrick Tanzania,Elly shimbi akiongea na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakati wa kongamano lakuwajengea uwezo wakujiamini na kuhimili ushindani wa ajira na kujiajiri lililoandaliwa na taasisi ya AIESEC Tanzania lililofanyika katika chuo hicho mwishoni mwa wiki kwaudhamini wa Barrick.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na vyuo vya elimu ya juu mkoani humo wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa kongamano hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa ,Mayeka Simon Mayeka akiongea katika kongamano hilo.
Na Mwandishi Wetu.

Kampuni ya madini ya Barrick nchini, imedhamini na kushiriki katika kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma na Iringa lililoandaliwa na taasisi ya kuchipua na kuendeleza vipaji vya uongozi kwa vijana (AIESEC Tanzania) lililofanyika katika vyuo hivyo na kuwashirikisha wanafunzi wanaosoma vyuo vya elimu ya juu,wahadhiri na wadau mbalimbali.

Kupitia makongamano haya ambayo hufanyika kila mwaka, wanafunzi huweza kufahamu jinsi taasisi mbalimbali nchini zinavyoendesha shughuli zake lengo kubwa ikiwa ni kuwajengea uwezo wa kujua vipaji walivyonavyo, kujifunza jinsi ya kujiamini na kukabiliana na ushindani katika soko la ajira,kujiamini kwa kujiajiri,kuchangamkia fursa zinazojitokeza na kujitambua uwezo wao ni jinsi gani wanaweza kushiriki kutoa mchango wa kuendeleza taifa pindi wamalizapo masomo yao.

Maofisa Raslimali Watu Waandamizi na wataalamu mbalimbali kutoka Barrick pia walishiriki katika maonesho na kongamano hayo ambapo walipata fursa kuzungumza na wanafunzi kuhusiana na kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ajira,kuendeleza vipaji vyao pia wanafunzi walipata fursa kuelewa jinsi kampuni ya kimataifa ya dhahabu ya Barrick, inavyoendesha shuguli zake kwa kutoa kipaumbele kusaidia jamii sambamba na mpango wake wa kuibua na ukuzaji wa vipaji kwa vijana wa kitanzania,kuwezesha wanawake kuingia katika sekta na wafanyakazi wake.

Wanafunzi kutoka vyuo hivyo walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusiana na ajira kwa wataalamu wa fani ya Raslimali kutoka makampuni mbalimbali walioshiriki katika makongamano hayo.

Akiongea katika kongamano lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa ,Mayeka Simon Mayeka ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka wanafunzi kujiamini wakati wote na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza zikiwemo za ajira na kujiajiri.
Alisema zama hizi na maisha ya kidigitali vijana wanayo nafasi kubwa kupata mafanikio iwapo wataandaliwa vizuri.Alipongeza taasisi ya AIESEC Tanzania kuandaa makongamano ya kuwajengea uwezo wanafunzi vyuoni pia aliipongezakampuni ya Barrick kwa kudhamini makongamano haya.
Wataalamu kutoka Barrick wakiongea katika kongamano la wanafunzi wa Chuo kikuu cha Iringa lililoandaliwa na na taasisi ya AIESEC Tanzania lililofanyika katika chuo hicho mwishoni mwa wiki kwa udhamini wa Barrick.
Dar es Salaam. Tarehe 27 Aprili 2024: Katika kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu nchini, Benki ya CRDB imeasaini mkataba wa ushirikiano na Chama cha Wawekezaji katika Elimu Tanzania (TAPIE) utakaowawezesha wanachama wake kupata mikopo nafuu ya kuboresha miundombinu na kuwezesha uendeshaji wakati wote.


Mkataba huo umesainiwa tarehe 27 Aprili 2024 kwenye mkutano mkuu wa 5 wa mwaka wa TAPEI uliofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt Doto Biteko na kuhudhuriwa na wadau wa elimu nchini.
Akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano mkuu huo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema Benki inatambua changamoto wanazokutana nazo wamiliki binafsi wa shule hivyo imechukua hatua za kusaidia kuzitatua ili kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi kusoma na kujifunza.


“Ni ukweli usiopingika kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa lolote lile duniani kwani husaidia kujenga maarifa, ujuzi na kuongeza ufanisi hivyo kuwa kichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi. Kwa kuyatambua haya yote, Benki ya CRDB imeiweka sekta ya elimu katika moja ya vipaumbele vyake vya uwezeshaji. Tunafanya hivi ikiwa ni sehemu za kusaidia jitihada za Serikali pamoja na wadau wa sekta hii kutoa elimu bora itikayozalisha rasilimali watu bora katika nyanja mbalimbali,” amesema Raballa.


Kwa kuzitambua changamoto zilizopo ukiwamo ukweli kwamba uendeshaji wa shule unategemea mapato yatokanayo na ada ambayo mara nyingi hukusanywa shule zinapofunguliwa hivyo kuwa na uhaba pindi zinapofungwa, Benki ya CRDB imewaletea mkopo wa uendeshaji ili kukidhi mahitaji yanayopaswa kulipiwa wakati mapato mengine yakisubiriwa indi muhula mpya utakapoanza.
Raballa pia amesema shule nyingi zipo kwenye maeneo ambayo hayajarasmishwa jambo linalowanyima wamiliki uwezo wa kukopa kutokana na kutokidhi vigezo vya dhamana hivyo Benki ya CRDB imewaletea suluhisho kwa kuwaruhusu kukopa fedha zitakazowezesha urasmishaji wa maeneo yao ili kupata hati ya wizara itakayowaruhusu kukopa ili kuimarisha biashara zao.


“Tunawaruhusu wamiliki wa shule kukopa mpaka shilingi milioni 10 kwa ajili ya kurasmisha maeneo ya shule. Fedha hizi ni kwa ajili ya kutafuta hati ya wizara hivyo kuyatambulisha maeneo yao ya kisheria. Vilevile, tunayo mikopo kwa dhamana zisizo rasmi yaani maeneo ya shule ambayo hayana hati. Benki yetu inamruhusu mmiliki kuja kukopa mpaka shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule. Tunaamini kwa utaratibu huu rahisi na rafiki, tutasaidia kuwezesha uwekezaji wa shule katika sekta binafsi,” amesema Raballa.
Wakati wamiliki wakipewa mkopo wa uwekezaji wanaoweza kuurejesha mpaka kwa miaka 7, Raballa amesema walimu na wafanyakazi wa shule binafsi nao wanaweza kupata mkopo kwa ajili ya kufanikisha mambo yao binafsi. Mikopo ya wafanyakazi hawa, amesema inajumuisha ‘salary advance’ ambao ni mahsusi kwa wale ambao mishahara yao inapitia Benki ya CRDB ambao wanaweza kupata mpaka asilimia 50 ya mshahara wao na wakalipa ndani ya siku 30 pamoja na mkopo wa binafsi unaofika mpaka shilingi milioni 100 zinazoweza kurejeshwa kwa mpaka miaka 8.


”Kwa miaka mitatu iliyopita, kiwango cha mikopo ya eimu tuliyoitoa kwa kundi hili imekuwa ikiongezeka. Mwaka 2021 Benki yetu ya CRDB ilikopesha zaidi ya shilingi bilioni 78.66 ambazo zilipanda mpaka shilingi bilioni 86 mwaka 2022 na mwaka jana zikawa shilingi bilioni 97.17. Nitumie fursa hii kuweka wazi kwamba mikopo hii tunayotoa kwa wamiliki wa shule binafsi hasa wanachama wa TAPIE, inaweza kurejeshwa mpaka kwa miaka 7,” amesisitiza Raballa.
Kwa upande wake, rais wa TAPIE, Mahmoud Mringo amesema hadi sasa kuna zaidi ya shule 6,362 zinazojumisha za awali 2,364, za msingi 2,270 na sekondari 1,728 zinazomilikiwa na watu binafsi, mashirika ya dini na yasiyo ya dini, majeshi, na jumuiya za wazazi ambazo zimedahili takriban wanafunzi 1,020,772 kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita ambazo zimeajiri takribani walimu 59,445 na wataalamumwengine zaidi ya 100,000 wenye taaluma na ujuzi mbalimbali kama wahasibu, madereva, wasimamizi na walezi wa wanafunzi, walinzi na wapishi. Ajira hizi zimesaidia kuinua hali za kimaisha kwa watu husika na kupanua wigo wa kodi mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa taifa.


“Ukitaka kujenga darasa, maabara au kuboresha miundombinu mingine ya shule, ni lazima uende kukopa benki lakini tatizo ni riba kubwa. Kujenga shule ndogo tu kwa sasa unahitaji walau shilingi bilioni 2 lakini kuwa na shule yenye kila kitu basi unahitaji shilingi bilioni 10. Ukizikopa hizi kutoka benki na ukalipa kwa riba iliyopo, itakuchukua miaka 20 ya kumaliza deni ambalo ni lazima lilipwe na mwanafunzi.


Bado kuna kodi na tozo 16 ambazo shule inatakiwa kulipa. Haya mambo yote yanaifanya elimu yetu kuwa ghali na kusoma shule zisizo za serikali inaonekana ni anasa,” amesema Mringo akiiomba serikali iangalie namna ya kupunguza riba ya mikopo tozo pamoja na kodi.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko amepongeza juhudi za sekta binafsi kuchangia kuboresha elimu nchini kwamba zinaifanya jamii iwe na mchango zaidi katika kukuza uchumi. "Niwapongeze kwa ushirikiano na mkataba wa makubaliano mnayosaini leo na Benki ya CRDB. Ili kufanikisha mambo, ushirikiano na wadau wengine ni muhimu sana. Hivi mnavyofanya, ndio namna nzuri ya kukabiliana na changamoto zetu," amesema Dkt Biteko.