Kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda atafanya ziara rasmi nchini kuanzia tarehe 5 hadi 6 Agosti 2026.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Museveni atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yatakayojikita katika kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika maeneo mbalimbali, ikiwemo biashara na uwekezaji, miundombinu na usafirishaji, nishati, utalii, masuala ya ulinzi na usalama, na mtangamano wa kikanda.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha zaidi mahusiano ya kihistoria, ya kindugu na ya kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda. Aidha, viongozi hao watapitia maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya pamoja na kujadili hatua za kuondoa vikwazo vinavyoathiri biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Baada ya mazungumzo rasmi, viongozi hao wawili wanatarajiwa kushuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) katika masuala ya nishati. Aidha, watazungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa pamoja ambapo wataeleza masuala yaliyojadiliwa, makubaliano na maamuzi yaliyofikiwa, pamoja na mwelekeo wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Ziara hiyo ni ya pili kwa Mheshimiwa Rais Museveni nchini Tanzania katika mwaka 2026, na itatoa fursa kwa viongozi hao kutathmini utekelezaji wa maamuzi yaliyokwishafikiwa kati ya Tanzania na Uganda, ikiwemo maazimio ya Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) uliofanyika mwezi Machi 2026. Vilevile, viongozi hao wanatarajiwa kutoa mwelekeo wa hatua za kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.



Toa Maoni Yako:
0 comments: