Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (kulia), wakipanda na kumwagilia mti katika Shule ya Msingi Usule, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, ikiwa ni sehemu ya shughuli za uwajibikaji kwa jamii zilizotekelezwa na Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, kilichozinduliwa mkoani Tabora tarehe 22 Julai 2026. Kama sehemu ya uzinduzi huo, Kampuni hiyo pia ilikabidhi madawati 100 kwa Shule ya Msingi Usule kwa lengo la kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati na kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora na salama ya kujifunzia, pamoja na kutoa magodoro 100 kwa Kituo cha Kulelea Watoto cha Istiqaama kwa ajili ya kuboresha mazingira ya maisha ya watoto wanaoishi katika kituo hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (katikati), akikata utepe kuzindua rasmi kituo cha 100 cha huduma za mafuta ya rejareja cha Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania nchini, kilichopo eneo la Usule, Mkoa wa Tabora. Kituo hicho ni cha kwanza cha Kampuni hiyo mkoani Tabora na kitawawezesha wakazi wa Tabora na maeneo jirani kupata huduma za mafuta, vilainishi vya Puma, gesi ya kupikia ya PumaGas pamoja na fursa za kujipatia pointi kupitia mpango wa Puma Pris. Uzinduzi huo ni sehemu ya upanuzi wa mtandao wa huduma za mafuta wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania unaolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati salama na ya uhakika nchini. Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 22 Julai 2026 ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Meya wa Manispaa ya Tabora, Mheshimiwa Gulam Dewji (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (wa pili kushoto), Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora, Bi. Asha Churu (wa pili kulia), pamoja na mmiliki wa kituo hicho, Bw. Kishimba Kibera (kulia).

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (kushoto), akipokea dawati kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (kulia), ikiwa ni sehemu ya madawati 100 yaliyotolewa na Kampuni hiyo kwa Shule ya Msingi Usule, iliyopo Kata ya Mbugani, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora. Msaada huo unaolenga kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati na kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora na salama ya kujifunzia ni sehemu ya shughuli za uwajibikaji kwa jamii zilizotekelezwa na Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania wakati wa uzinduzi wa kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, kilichozinduliwa mkoani Tabora tarehe 22 Julai 2026.
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Nishati ya Puma Tanzania imezindua rasmi kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, huku ikifungua kituo chake cha kwanza mkoani Tabora katika hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati salama na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Kituo hicho kilichopo mjini Tabora kilizinduliwa Julai 22, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, akishirikiana na viongozi wa serikali, wawakilishi wa wananchi, wateja pamoja na menejimenti ya kampuni hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Tanzania, Fatma Abdalla, alisema kufikisha vituo 100 ni ishara ya imani ya kampuni katika uchumi wa Tanzania na dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati.
Alisema uwekezaji huo utarahisisha upatikanaji wa mafuta ya uhakika, kuimarisha biashara, kuchochea shughuli za usafirishaji na kuongeza fursa za ajira, hususan katika mkoa wa Tabora ambao unaendelea kukua kwa shughuli za kilimo na biashara.
"Kuanzisha kituo chetu cha 100 si tu kupanua mtandao wa huduma, bali ni kuimarisha ushirikiano wetu wa muda mrefu na Tanzania. Tunaamini upatikanaji wa nishati ya uhakika unafungua fursa za maendeleo kwa wananchi na uchumi wa taifa," alisema Abdalla.
Mbali na uwekezaji huo, kampuni hiyo ilitekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikitoa magodoro 100 kwa Kituo cha Kulelea Watoto cha Istiqaama, madawati 100 kwa Shule ya Msingi Usule pamoja na kupanda miti 100 kwa kushirikiana na wananchi ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, aliipongeza Puma Tanzania kwa kuendelea kuwekeza nchini, akisema hatua hiyo itaongeza ajira, kuimarisha biashara za ndani na kuchangia maendeleo ya mkoa huo.
Alisema uwekezaji wa kampuni hiyo unaonesha imani ya wawekezaji katika mazingira ya biashara nchini na kuwataka wawekezaji wengine kutumia fursa zilizopo mkoani Tabora.
Puma Tanzania ni sehemu ya Kampuni ya Nishati ya Puma inayofanya shughuli zake katika zaidi ya nchi 34 duniani, ikitoa huduma za usambazaji wa mafuta, mafuta ya anga, vilainishi na lami kwa kuzingatia viwango vya usalama, ubora na maendeleo endelevu.




Toa Maoni Yako:
0 comments: