Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya
akizungumza na kwenye Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero
za ardhi za wananchi wa Kijiji cha Msonge, Kata ya Mvuha, Wilayani
Morogoro, tarehe 30 Mei 2026.Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka wananchi kote nchini kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuvamia maeneo yaliyotengwa kisheria kwa ajili ya uwekezaji, akisisitiza kuwa hatua hizo zinakiuka sheria za nchi na kurudisha nyuma maendeleo.
Mhe. Mmuya ametoa kauli hiyo tarehe 30 Mei 2026, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za ardhi za wananchi wa Kijiji cha Msonge, Kata ya Mvuha, Wilayani Morogoro.
Katika mkutano huo, Mhe. Mmuya alisisitiza kuwa wananchi wasiende kuvamia eneo ambalo tayari limekabidhiwa kwa mwekezaji, kwani kufanya hivyo ni kuingilia haki za mtu mwingine, na kuongeza kuwa kama mwekezaji ana hati na nyaraka halali, basi wanakijiji hawapaswi kuvamia maeneo waliyoyatenga wenyewe kwa ajili ya uwekezaji.
Akifafanua kuhusu chanzo cha mgogoro huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Msonge Aloyce Banzi alieleza kuwa serikali ya kijiji ilitenga eneo la ekari 1,600 kwa ajili ya uwekezaji, kwa makubaliano ya kwamba wawekezaji hao wangejenga jengo la maabara ya kijiji.
Hata hivyo, kutokana na changamoto zilizokuwa nje ya uwezo wao, wadau hao walishindwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati, hali iliyosababisha uongozi kusuasua kuwakabidhi eneo hilo rasmi.
Kwa upande mwingine, mmoja wa wakulima wanaoomba eneo hilo kwa ajili ya kilimo cha kimkakati cha Alizeti na Michikichi, Bw. Philipo Petro Nanyaro, alisema wamekuwa wakifuatilia eneo hilo kwa muda mrefu bila kupata suluhisho la kudumu. Bw. Nanyaro alibainisha kuwa, ingawa walitarajia kukabidhiwa ardhi hiyo, mchakato huo umekwama kisheria huku kukiwa na jengo la maabara ambalo ujenzi wake umesimama kutokana na changamoto za kiutawala na kimaslahi.
Mara baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwataka wakulima hao kutimiza wajibu wa makubaliano yao na kijiji, huku akiutaka uongozi wa kijiji kurejea taratibu za kisheria za ugawaji wa ardhi ili kujiridhisha kama sheria inatoa mamlaka kwa kijiji kugawa ekari zote hizo 1,600.
Ziara hiyo ya Naibu Waziri Kaspar Mmuya mkoani Morogoro ilikuwa na malengo makuu matatu ikiwemo kukagua shamba la Morogoro Sugar ikiwa ni sehemu ya kutekeleza ahadi aliyoitoa bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Mhe. Zuberi Yahya Mfaume kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi. Lengo lingine lilikuwa ni kufanya mikutano ya hadhara ili kusikiliza na kutatua changamoto za ardhi zinazowakabili wananchi, pamoja na kugawa Hati za Hakimiliki za Kimila 2104 kwa wakazi wa Kijiji cha Bwakila Chini, Nyarutanga, Gomero, Kichangani na Mgazi Kata ya Mbwade na Hati za kawaida 30 kwa wananchi wa Kijiji cha Dutumi.




Toa Maoni Yako:
0 comments: