Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Tanzania Breweries Limited (TBL) imetoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kushirikiana kwa karibu katika kukabiliana na changamoto ya pombe haramu, ikisema tatizo hilo linaendelea kuhatarisha afya ya wananchi, kudhoofisha uchumi na kuathiri biashara halali.
Akizungumza katika taarifa yake, kampuni hiyo imepongeza juhudi za Serikali zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya biashara haramu, hususan operesheni za kukamata na kuondoa bidhaa bandia sokoni, ambazo zimeelezwa kuwa zinaonesha dhamira ya kulinda watumiaji na kuhakikisha ushindani wa haki.
Hata hivyo, TBL imebainisha kuwa pombe haramu bado imeenea kwa kiwango kikubwa nchini, hali inayowaweka wananchi wengi katika hatari ya kutumia vinywaji visivyo salama na visivyodhibitiwa. Imeelezwa kuwa hali hiyo pia inaongeza shinikizo kwa sekta ya afya na kudhoofisha uchumi rasmi.
Kwa upande wa afya, imeelezwa kuwa pombe haramu mara nyingi hutengenezwa bila kufuata viwango vinavyotakiwa, jambo linaloweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo uharibifu wa viungo vya mwili, kupoteza uwezo wa kuona na hata vifo.
Kiuchumi, TBL imeeleza kuwa Tanzania inapoteza zaidi ya shilingi trilioni moja kila mwaka kutokana na mapato yasiyokusanywa yanayotokana na biashara hiyo haramu. Fedha hizo zingeweza kusaidia kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu na miundombinu.
Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuwa uwepo wa pombe haramu unaathiri ushindani wa haki sokoni, kwani wafanyabiashara wanaofuata sheria hukumbana na ushindani kutoka kwa wale wanaokwepa kodi na kuuza bidhaa kwa bei ya chini, hali inayopunguza uwekezaji na kuathiri ajira.
Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, amesema kuwa suluhisho la kudumu linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla. Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha utekelezaji wa sheria, kuweka mifumo madhubuti ya udhibiti, pamoja na kuendesha kampeni za elimu kwa umma kuhusu madhara ya pombe haramu.
“Mapambano dhidi ya pombe haramu ni jukumu la pamoja. Kila mdau ana nafasi ya kuhakikisha bidhaa zisizo salama zinapungua sokoni na wananchi wanatumia bidhaa zilizo salama na zinazokidhi viwango,” alisema Kilpin.
TBL imeeleza kuwa itaendelea kujikita katika uzalishaji wa bidhaa bora pamoja na kushirikiana na wadau wengine katika kulinda afya ya watumiaji na kukuza matumizi ya uwajibikaji.
Imeelezwa kuwa pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa, bado kuna haja ya kuweka mikakati ya muda mrefu itakayohakikisha tatizo la pombe haramu linadhibitiwa kikamilifu, hasa kwa kuzingatia kuwa upatikanaji wake kwa urahisi na bei nafuu unaendelea kuchochea matumizi yake kwa baadhi ya makundi ya wananchi.
Mapambano dhidi ya pombe haramu yameainishwa kuwa muhimu katika kulinda afya ya jamii, kuongeza mapato ya Serikali na kuhakikisha soko la pombe linakuwa salama, lenye ushindani wa haki na endelevu.



Toa Maoni Yako:
0 comments: