Muongo mmoja wa ushirikiano na Serikali na kufanya uwekezaji wa TZS bilioni 2.5 katika miradi ya maji vijijini na SBL inaendelea kufanya uwekezaji huo.
KARATU, 30 APRILI 2026: Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) leo imeandika historia muhimu kwa kukamilisha mradi wake wa 30 wa maji safi na salama nchini Tanzania, uliozinduliwa rasmi katika Kata ya Baray, Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha. Hafla hiyo imeongozwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Eng. Kundo A. Mathew. (Mb)
Mradi wa maji wa Baray ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa SBL katika sekta ya maji, ukinufaisha zaidi ya wakazi 15,000 wa eneo hilo kwa maji safi na salama. Mradi huu una uwezo wa kuzalisha hadi mita za ujazo 110,632 kwa mwaka. Mradi huu umegharimu kiasi cha TZS milioni 344, zilizofadhiliwa kikamilifu na SBL, kwa kushirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Africa Community Advancement Initiative (Africai).
Baray ni miongoni mwa miradi mitatu iliyokamilishwa na SBL mwaka huu, mingine ikiwa ni katika Kata ya Kambi ya Simba (Karatu) na Kata ya Ihushi (Mwanza). Kwa pamoja, miradi hii inawakilisha uwekezaji wa TZS milioni 655 kwa mwaka wa fedha 2026, ukiwanufaisha watu 23,189 na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji safi wa mita za ujazo 169,279 kwa mwaka.
Hadi sasa, SBL imewekeza takribani TZS bilioni 2.5 katika miundombinu ya maji vijijini nchini Tanzania, ikiwa imewafikia zaidi ya watu milioni 2.3.
Mpango wa “Water for Life” wa SBL umejengwa kwa kuendana moja kwa moja na Sera ya Taifa ya Maji (NAWAPO), ambayo inalenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kupanga, kujenga, kuendesha, kutunza na kusimamia miradi ya maji ya jamii. Kila mradi wa SBL huanza kwa kujenga umiliki wa jamii, kwa kushirikiana kwa karibu na RUWASA, mamlaka za wilaya na vyombo vya usimamizi wa maji vya kijamii ili kuhakikisha miradi inabaki endelevu hata baada ya uzinduzi.
Mradi wa Baray unajumuisha pampu za kisasa za kuzamishwa majini (submersible pumps), nyumba za pampu, matenki ya kuhifadhia maji, mtandao wa mabomba ya usambazaji, vituo 20 vipya vya kuchotea maji, pamoja na ukarabati wa vituo 15 vilivyokuwepo awali, miundombinu ambayo sasa ni mali ya jamii inayohudumiwa.
Pamoja na miundombinu hiyo, SBL na Africai wametekeleza programu ya mafunzo ya “Women in Water, Sanitation and Hygiene (WASH)”, iliyowawezesha wanawake 30 kutoka Baray na Kambi ya Simba kupata ujuzi wa kiufundi wa matengenezo ya miundombinu ya maji na ulinzi wa vyanzo vya maji, ujasiriamali katika utengenezaji wa sabuni, elimu ya fedha na masoko, pamoja na mafunzo ya uongozi na uelewa wa ukatili wa kijinsia.
Mpango huu unaakisi imani ya msingi ya SBL kwamba maji safi ni msingi wa maendeleo ya jamii, lakini ushirikishwaji wa kiuchumi ndio unaoifanya iwe endelevu.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Eng. Kundo Mathew, aliipongeza SBL kwa mchango wake na kuhimiza ushirikiano zaidi wa sekta binafsi.
“Serikali inaendelea kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama, lakini juhudi hizi zinahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali. Tunathamini sana mchango wa sekta binafsi kama Kampuni ya Bia ya Serengeti katika kusaidia kufikia malengo haya ya kitaifa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Dkt. Obinna Anyalebechi, alisema hatua hiyo ni kielelezo cha dhamira ya muda mrefu ya kampuni kwa nchi.
“Miradi 30 ya maji si namba tu bali ni jamii 30 ambazo maelfu ya wasichana hawalazimiki tena kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hivyo wanaweza kwenda shule; ni akina mama wanaopata muda wa kujenga biashara zao; na ni vituo vya afya vinavyoweza kutoa huduma kwa usalama. Mradi wa Baray ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi tuliyowahi kutekeleza, na unatukumbusha kwa nini tulianza na kwa nini hatuachi. Sisi ni biashara ya Kitanzania, na mafanikio yetu hupimwa kwa nchi tunayojenga,” alisema.
Mkurugenzi wa Africai, Dkt. Bonus Caesar, aliongeza: “Ushirikiano huu umetuwezesha kutoa huduma muhimu kwa jamii kwa njia endelevu. Tumejipanga kuhakikisha miradi hii si tu inatekelezwa, bali pia inasimamiwa ili ilete manufaa ya muda mrefu kwa jamii. Tunashukuru SBL kwa ushirikiano wake.”
SBL ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa nchini Tanzania na mchango wake katika uchumi wa taifa ni mkubwa. Hata hivyo, mchango wake hauishii kwenye kodi pekee, bali unaonekana katika visima vilivyochimbwa, wakulima wanaonufaika na soko, ajira zinazozalishwa na uwekezaji unaofanywa katika jamii.
Mradi wa Baray pia unasaidia moja kwa moja dira ya maendeleo ya Taifa ya Tanzania Vision 2050, inayolenga kuhakikisha angalau asilimia 85 ya wananchi wa vijijini wanapata maji safi na salama. Aidha, unatarajiwa kusaidia wakulima wa mahindi wa eneo la Karatu, wakiwemo wanaosambaza bidhaa kwa SBL.
“Wajibu wetu kwa Tanzania umejengwa kwenye nguzo tatu,” aliongeza Dkt. Anyalebechi. “Kodi tunazolipa, ajira tunazotengeneza, na uwekezaji katika jamii. Biashara endelevu na inayokua ndiyo inayowezesha nguzo hizi zote. Nguzo moja ikidhoofika, zote zinaathirika, na hivyo pia maendeleo tunayojenga pamoja na Serikali.”
Kadri Tanzania inavyojiandaa kwa malengo mapya ya mipango ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/27, SBL imeeleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Serikali katika sera zinazosaidia ustahimilivu wa sekta na mapato ya taifa. Mazingira ya kodi yaliyo thabiti na yenye uwiano yanaruhusu uwekezaji wa muda mrefu unaoleta matokeo kwa jamii na miundombinu ya maji, mapato ya kodi, ajira rasmi na ukuaji wa uchumi unaohitajika nchini Tanzania.










Toa Maoni Yako:
0 comments: