Na Mwandishi Wetu

Tasnia ya filamu nchini imepata pigo kufuatia kifo cha msanii mkongwe, Mzee Kambi, kilichotokea leo Aprili 27, 2026.

Taarifa za kifo hicho zimethibitishwa na Msemaji wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Coletha Raymond, aliyesema kuwa msanii huyo alifariki dunia ghafla alipokuwa akiendelea na shughuli zake za kazi.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Coletha alisema Mzee Kambi alikuwa ametoka mkoani Tabora kikazi na aliporejea alielekea moja kwa moja katika shughuli zake kwenye studio za Pilipili, kabla ya kuanza kujisikia vibaya.

“Ni kweli tumempoteza Mzee Kambi. Alikuwa ametoka Tabora na alipofika alienda moja kwa moja kazini katika studio za Pilipilibl. Akiwa kazini ndipo alipozidiwa ghafla na kukimbizwa hospitali, lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia,” alisema Coletha.

Aliongeza kuwa chanzo cha kifo kinahusishwa na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yakimsumbua, ikiwemo presha na kisukari.

Aidha, alisema Shirikisho la Filamu Tanzania linaendelea na taratibu za ndani kwa kushirikiana na familia ya marehemu ili kupanga mipango ya mazishi, ambapo taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Kifo cha Mzee Kambi kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu nchini, ambapo amekuwa mmoja wa wasanii waliotoa mchango mkubwa katika kukuza sanaa hiyo kwa muda mrefu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: