Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha wanadumisha umoja, upendo na amani nchini, akisisitiza kuwa maandamano, vurugu na uvunjifu wa amani havina faida yoyote bali huleta maumivu kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Samia alitoa kauli hiyo mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Tanzania, katika hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Gwaride, Jijini Dodoma, kufuatia ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na kuheshimu sheria za nchi, huku akionya wale wanaoshawishi au kuratibu ghasia katika baadhi ya mikoa kwa lengo la kuharibu utulivu wa Taifa.

“Hatuna budi kuhakikisha tunahimizana umoja na upendo kwa nchi yetu. Tunadumisha amani na kuheshimu sheria za nchi. Kinyume cha hayo, maandamano, vurugu na uvunjifu wa amani husababisha maumivu na havileti manufaa wala faida kwa yeyote,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alisisitiza pia umuhimu wa busara na hekima katika kutatua changamoto za kijamii na kisiasa, akiwataka Watanzania kuchagua njia ya upendo, uvumilivu na unyenyekevu badala ya chuki, hasira na mgawanyiko.
“Niwasihi Watanzania, tuchague hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemko, upendo badala ya chuki, uvumilivu badala ya vinyongo, umoja badala ya mgawanyiko, na amani badala ya vurugu. Ni wajibu wetu pia kuchagua unyenyekevu badala ya kiburi, na huruma badala ya hasira,” aliongeza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alisisitiza kuwa Tanzania ni moja na hakuna aliye na nguvu kuliko Taifa, akibainisha kuwa kipimo cha kweli cha demokrasia si ushindi katika uchaguzi, bali ni jinsi Taifa linavyosimamia umoja na maridhiano baada ya uchaguzi.

“Taifa letu litakuwa na nguvu zaidi pale ambapo sauti zote zitakaposikilizwa na kuheshimiwa. Huu ni wajibu wa kila mmoja wetu na wa taasisi zote kuhakikisha maumivu ya Watanzania yanaponywa,” alisema.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia aliwashukuru viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali kwa mchango wao mkubwa katika kuhimiza amani, upendo na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Alimalizia kwa kuagiza kurejea kwa shughuli zote za kijamii na kiuchumi katika hali ya kawaida, akiwahakikishia Watanzania kuwa nchi ipo salama na serikali itaendelea kulinda amani, usalama na ustawi wa wananchi wake.

“Tanzania ni nchi ya amani. Tutailinda amani hii kwa vitendo, kwa mshikamano, na kwa kuheshimiana,” alisema Rais Samia.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: