Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi nchini limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa kikundi cha watu wanaodaiwa kuandaa na kusambaza taarifa, picha mjongeo na video za matukio ya uongo mitandaoni kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi kuelekea siku ya kupiga kura kesho, Oktoba 29, 2025.
Taarifa ya Jeshi hilo imeeleza kuwa kundi hilo limekuwa likitumia matukio ya zamani ambayo Polisi walishayashughulikia, pamoja na kutunga matukio mapya, ili kuonyesha kana kwamba yametokea hivi karibuni, na hivyo kujaribu kuleta taharuki miongoni mwa wananchi.
Akizungumza na vyombo vya habari, Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP David Misime, amewataka wananchi kuwa makini na taarifa hizo zisizo sahihi, akisisitiza kuwa lengo la wahusika ni kuchonganisha na kugombanisha watu ili kudhoofisha amani ya taifa.
“Wapo pia walioandaliwa kutoa taarifa zenye tungo tata, zenye nia ya kuleta taharuki. Wanakusanya matukio yaliyotokea katika nchi nyingine na kuyawekea sauti za Kiswahili ili yaonekane yanatokea hapa nchini,” alisema Misime.
Ameongeza kuwa jeshi hilo pia limebaini uwepo wa mipango ya kuchukua picha za baadhi ya viongozi na kuziwekea maneno au sauti zenye matamko ya upotoshaji, ili kuonyesha kana kwamba viongozi hao wameyasema mambo ambayo si ya kweli.
Misime alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuhakikisha usalama wa kutosha nchini kote kuelekea uchaguzi, na hakuna tishio lolote la kiusalama kama lilivyothibitishwa katika taarifa yao ya Oktoba 26, 2025.
Aidha, amewataka wananchi kupuuza na kufuta mara moja taarifa, picha au video za aina hiyo zitakazotumwa kwao, badala ya kuzisambaza, kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao.
“Tunatoa rai kwa wananchi wote kuwa watulivu, wasiamini kila wanachokiona mtandaoni, na waendelee kujitokeza kwa wingi kesho kupiga kura kwa amani,” alihitimisha Misime.



Toa Maoni Yako:
0 comments: