Na Mwandishi Wetu, Geita

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amezindua Mpango wa Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Vijana (YEE) utakaowanufaisha zaidi ya vijana 12,000 katika maeneo yanayopitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika Bukombe mkoani Geita, Dkt. Biteko alisema mpango huo unalenga kuongeza ujuzi, kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, na kuondoa vikwazo vya ujasiriamali kwa vijana.

“Kampuni zinazotekeleza miradi nchini zisitoe tu ujuzi, bali pia zitoe mitaji ili vijana wafanye vizuri zaidi. Tunataka ujuzi unaotolewa uende sambamba na mtaji,” alisema.

Katika awamu ya kwanza, mpango huo utawafikia wanawake 6,130, wanaume 4,905 na makundi maalum 1,226 katika mikoa ya Geita, Kagera, Tabora na Tanga. Awamu ya pili itahusisha mikoa ya Singida, Shinyanga, Dodoma na Manyara.

Dkt. Biteko alibainisha kuwa tangu kuanza kwa mradi wa EACOP mwaka 2022, zaidi ya Watanzania 9,194 wamepata ajira za moja kwa moja, huku wengine 238 wakipatiwa ufadhili wa masomo katika vyuo mbalimbali.

Aidha, aliwataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na miradi ya kimkakati huku akisisitiza nidhamu na uaminifu. “Vijana wakipata nafasi wanapaswa kujituma na kuwa waaminifu, serikali itaendelea kutengeneza fursa zaidi za kiuchumi kwao,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Mhe. Patrobas Katambi, alisema mpango huo ni kielelezo cha juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha vijana wanapata ajira na mitaji.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, alisema wananchi wa Geita wamenufaika na EACOP kupitia ajira za muda mfupi na mnyororo wa thamani wa biashara mbalimbali.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, alieleza kuwa mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi 17 mikubwa inayotekelezwa na wizara hiyo, ukiwa na thamani ya trilioni 1.325 zinazolipwa kwa kampuni za Kitanzania zinazoshiriki utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Meneja Uwekezaji na Uwajibikaji kwa Jamii wa EACOP, Clare Haule, alisema zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wako chini ya miaka 35, na mpango wa YEE umebuniwa mahsusi kupunguza changamoto za ajira na ujasiriamali zinazowakabili vijana wengi hususan vijijini.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: