Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bi. Sakina Mwinyimkuu, amewataka watumishi wa umma waliopata mafunzo ya ufuatiliaji na tathmini kutumia maarifa hayo kuboresha utendaji kazi na kuongeza uwajibikaji katika taasisi zao.
Akizungumza jijini Dodoma tarehe 25 Julai, 2025 wakati wa kufunga mafunzo ya siku tano kwa watumishi wa umma, Bi. Sakina alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia utendaji unaozingatia matokeo (results-based performance).
“Mafunzo haya si kwa manufaa yenu binafsi pekee, bali ni nyenzo ya kuleta mabadiliko chanya katika taasisi zenu. Ni wajibu wenu kuyaishi na kuyatumia kikamilifu kwa manufaa ya umma,” alisema Bi. Sakina.
Aidha, aliwahimiza washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa kueneza maarifa waliyojifunza kwa wenzao katika maeneo yao ya kazi, kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia viwango vya kitaifa vya ufuatiliaji na tathmini ya maendeleo.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika kusimamia, kupima na kuripoti matokeo ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa waandaaji, programu hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha utekelezaji wa mipango ya kitaifa unafuatiliwa kwa karibu na kuleta tija kwa wananchi.











Toa Maoni Yako:
0 comments: