Dodoma, Februari 7, 2025 – Benki ya CRDB imefanikiwa kusaini mkataba wa kusimamia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayolenga kuwainua wanawake, vijana, na makundi maalum.

Kupitia mpango huu, Benki ya CRDB itasimamia mikopo katika halmashauri tano: Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Dodoma, Manispaa ya Kigoma, Halmashauri ya Mji wa Mbulu, na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa ameishukuru serikali kwa imani waliyoipa benki hiyo. Ameeleza kuwa uzoefu wa Benki ya CRDB na taasisi yake ya CRDB Bank Foundation katika usimamizi wa fedha na uwezeshaji wa wananchi utasaidia kuboresha usimamizi wa mikopo hiyo.

“Mpango huu unaendana moja kwa moja na jitihada zetu kupitia programu ya IMBEJU inayolenga kuwainua wajasiriamali wadogo. Tutatoa elimu ya fedha, ushauri wa biashara, na kuhakikisha mikopo inawafikia walengwa kwa uwazi na ufanisi,” alisema.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, alisisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua kali viongozi wa mikoa na wilaya watakaobainika kuhusika katika utoaji wa mikopo kwa vikundi hewa.

“Fedha hizi ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, hivyo lazima zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa. Wakuu wa mikoa na wilaya ambao wataruhusu uwepo wa vikundi hewa watawajibika moja kwa moja. Wananchi wanapaswa kuwa waaminifu kwa kurejesha mikopo yao ili mpango huu uwe endelevu,” alisema Mhe. Mchengerwa.
Ameongeza kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 234 zinatarajiwa kutolewa kwa wananchi kupitia njia mbili: mikopo inayosimamiwa na benki katika halmashauri 10 na mikopo iliyoboreshwa katika halmashauri 174 nyingine.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, alieleza utayari wa kushirikiana na Benki ya CRDB kuhakikisha mpango huu unafanikiwa. Aliwataka wananchi wa Dodoma na maeneo mengine kunufaika na mikopo hii kwa kuwekeza katika miradi endelevu.

Benki ya CRDB inajivunia kuwa sehemu ya mpango huu muhimu unaolenga kuinua uchumi wa wananchi na kukuza ujumuishi wa kifedha nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (kulia) akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: