Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Profesa Joyce Ndalichako, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi PSSSF wakati akilizindua Baraza la Pili mjini Morogoro Februari 2, 2023
NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan la kulipa wastaafu mafao kwa wakati.
Prof.Ndalichako ameyasema hayo leo Februari 2, 2023 mjini Morogoro alipokuwa akizindua Baraza la pili la wafanyakazi wa mfuko wa PSSSF.
“Mlitumie baraza hili kuhimiza kila mfanyakazi ajue wajibu wake ili kuuwezesha mfuko kusonga mbele katika kutekeleza maagizo ya serikali pamoja na kutoa huduma bora kwa wanachama,”amesema.
Aidha, amesema Mhe.Rais ameendelea kushughulikia changamoto za wastaafu ikiwa ni pamoja na kuwataka watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii kulipa mafao watumishi walioondolewa kazini kwa kubainika kuwa na vyeti feki.
“Kulikuwa na jumla ya watumishi Elfu Kumi na Nne (14,000) ambao waliondolewa kwenye utumishi kwa sababu ya vyeti feki, tayari watumishi 6,892 wameshalipwa na 3,169 bado madai yao yanafanyiwa kazi,” Alifafanua.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, amesema kwasasa mafao hayo ya wastaafu wanalipwa ndani ya siku 60 na uhakiki wa wastaafu unafanyika kidigitali.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko kwa nusu mwaka toka Julai 2022 hadi Desemba 2022, CPA Kashimba alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa aliyofanya ya kuhakikisha watanzania wengi wanapata ajira.
“Tumevuka lengo la kuandikisha wanachama kwa asilimia 270%, lengo letu lilikuwa kuandikisha wanachama 13,000, lakini tumevuka lengo hilo na kuandikisha wanachama 33,534, sisi wanachama wetu wanategemea jinsi serikali inavyoajiri, watu wengi wameajiriwa katika kipindi hicho.” Alisema.
Eneo lingine ambalo Mfuko umefanya vizuri ni makusanyo ya Michango ambapo lengo lilikuwa ni kukusanya Shilingi Bilioni 792 lakini Mfuko umeweza kukusanya Shilingi Bilioni 823 na hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 104%.
Kuhusu mapato yatokanayo na uwekezaji unaotokana na vitega uchumi, CPA Kashimba alisema Mfuko uliweka lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 256 na badala yake Mfuko umeweza kukusanya Shilingi Bilioni 297 na hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 116%.
Baraza hilo linalofanyika kwa siku mbili, limechagua viongozi wapya wakiwemo Katibu wa Baraza Bw. Steven Biko na Katibu Msaidizi Linda Njoolay.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (aliyesimama) akizungumza wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye ukumbi WA Magadu mjini Morogoro Februari 2, 2023. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba na kulia ni Katibu wa Baraza, Steven Biko.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PSSSF, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu, CPA Hosea Kashimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa baraza hilo
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PSSSF, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu, CPA Hosea Kashimba (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, (PSSSF), Bw. Paul Kijazi.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza wakisikiliza kwa makini wakati mkutano ukiendelea.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza wakisikiliza kwa makini wakati mkutano ukiendelea.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza wakisikiliza kwa makini wakati mkutano ukiendelea.
Baadhi ya watendaji wa PSSSF.
Mjumbe akinakili masuala muhimu yaliyozungumzwa.
Katibu wa Baraza Steven Biko.
Katibu Msaidizi wa Baraza Linda Njoolay.
Toa Maoni Yako:
0 comments: