Na Mohammed Hammie

“NINAPOKOSA msaada na hakuna maji, nikienda chooni huwa nakanyaga kinyesi au mkojo. Na kwa kuwa naishi nyumba ya kupanga, mara nyingi choo kikiwa kimechafuka, basi kila mmoja anajua ni mimi ndiye niliyefanya uchafu ule,” anasema Bi Christina Paul Chibalua, mlemavu wa macho anayeishi kata ya Chamwino, mtaa wa Msufini mkoani Morogoro.

Mwanamke huyu anaingia kwenye maadhimisho ya ‘Siku ya Choo’ akiishi katika mazingira ambayo choo ni tatizo kubwa kwake.
Bi Christina Paul Chibalua, mlemavu wa macho anayeishi kata ya Chamwino, mtaa wa Msufini mkoani Morogoro.
---
Novemba 19 kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya choo huku kauilimbiu ya mwaka huu ikiwa: ‘Kufanya yasiyoonekana yaonekane’. Hii ni kaulimbiu inayoangazia jinsi vyoo visivyo na ubora na mifumo duni inavyoathiri afya za watu na kuchafua mazingira, kupitia maji ya chini ya ardhi.

Hata hivyo makala hii imejikita kutazama hali ya usafi wa mazingira na athari zake hasa kwa wanawake na watu wenye ulemavu nchini Tanzania, mkoani Morogoro.

Lengo la Maendeleo Endelevu 6.2, linatoa ujumbe muhimu kwamba kila mtu lazima apate choo safi, salama na chenye usawa kwa wote kwa kuzingatia mahitaji ya wanawake na wasichana na wale walio katika mazingira hatarishi.

Hata hivyo, ujumbe huu unaweza usiwe na maana kubwa kwa Bi Christina Paul na wengine wanaoishi katika mazingira kama yake ukizingatia imesalia miaka minane pekee kufikia 2030, ikiitaka dunia kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kufikia lengo hilo.

Bi Christina anasema si kadhia ya usafi wa mazingira ya choo pekee anayoipata, bali pia kitendo cha kuchangia choo kimoja na wanaume kunamkososha hali ya kujiamini na kuushusha thamani ya utu wake kama mwanamke.

“Kukiwa hakuna watu na nimeshikwa na haja inanilazimu kwenda chooni kwa kupapasa ukuta. Nikiwa huko huwa napata hisia lazima kuna mtu ananitazama kwa siri kwani hata miundombinu ya choo sio mizuri,” anasema.

Mwanamke huyo ambaye anaishi bila mume, anasema wakati wa usiku huwa ni changamoto zaidi anapohitaji kwenda chooni kwa kuhofia kufanyiwa vitendo vya ukatili kwani choo wanachotumia kipo nje.

“Laiti ningelikuwa na mume huenda angelikuwa ananisindikiza, lakini sina. Huwa napata hofu kutoka nje usiku peke yangu lakini nikibanwa na haja ninakuwa sina namna nyingine,” anasema Bi Christina.

Shirika la WaterAid linaamini ukosefu wa vyoo huathiri faragha za wanawake na wasichana pamoja na usalama wao.

Ingawa ulemavu wa macho unaongeza tatizo kwa Bi Christina, lakini wapo wanawake na wasichana ambao mara nyingi husubiri hadi giza liingie ili wapate mahali tulivu pa kujisaidia katokana na mazingira ya vyoo wanavyotumia, hali inayoongezea hatari ya kunyanyaswa au hata kushambuliwa kingono.

Ili kuleta mabadiliko katika suala zima la huduma muhimu ya choo, ni muhimu upatikanaji wa maji na usafi na mazingira viwe kipaumbele sambamba na uwapo wa vyoo bora kwa kila mtu, kila mahali.

Hata hivyo, si kila mahali watu wanatilia maanani umuhimu wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira japokuwa ni haki ya binadamu inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.
Athumani Ally Kapate, mkazi wa kata ya Mazimbu, mtaa wa Modeko B, mkoani Morogoro ambaye ni mlemavu wa viungo.
---
Athumani Ally Kapate, mkazi wa kata ya Mazimbu, mtaa wa Modeko B, mkoani Morogoro ambaye ni mlemavu wa viungo, anasema mara kwa mara anapata maradhi ya tumbo na amekuwa akiwaeleza madaktari kwamba hali hiyo inatokana na kukosa maji ya kutosha kwa ajili ya kusafisha mazingira ya chooni.

“Naathirika kiafya, hasa kuumwa na tumbo, nikiulizwa na daktari hospitali huwa namueleza ukweli kuwa hali yangu ya ulemavu inanifanya niwe nashika chini ili niweze kupata huduma, lakini maji yaliyopo hayakidhi mahitaji ya huduma,” anasema Athumani ambaye kitaaluma ni mwalimu.

Kwa Athumani si nyumbani pekee anapokutana na changamoto ya usafi wa mazingira ya choo, bali pia eneo analofanyia kazi.

“Mashuleni pia kumekuwa na mikakati mingi ya kujengwa kwa vyoo. Wataalamu wanapokuja huwa wanauliza idadi tu ya matundu, lakini wanasahau je matundu hayo ya vyoo huwa ni rafiki kwa wanafunzi walemavu au waalimu wenye ulemavu katika shule husika (kama mimi)?” Anasema Mwalimu Ally.

Anasema mbali na mashuleni, anahimiza kujengwa vyoo rafiki kwa watu wote wakiwemo walemavu katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vile stendi za mabasi, kwenye masoko, nyumba za ibada na hata za starehe.

Siku ya choo duniani inagusa takribani watu bilioni 3.6 ambao bado wanaishi na vyoo duni ambavyo kushusha utu wao, vinaharibu afya zao na kuchafua mazingira yao.

Mashirika mbalimbali ulimwenguni yamekuwa yakifanya jitihada za makusudi katika kumaliza changamoto hiyo ya usafi wa mazingira, miongoni mwa mashirika hayo ni WaterAid.

Mkurugenzi mkazi wa shirika hilo nchini, Bi Anna Mzinga amesema WaterAid imekuwa ikishirikiana na serikali, kampuni, mashirika ya kijamii, wafanyabiashara na wajasiriamali, na watu wa jamii mbalimbali katika kuifikia jamii kwa ajili ya suala zima la usafi wa mazingira.

“Kimsingi tunashughulikia msururu mzima wa usafi wa mazingira ili kuhakikisha kuwa kinyesi cha binadamu kinadhibitiwa kwa usalama, ikijumuisha usafirishaji au uhifadhi,” anasema.
Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, Bw. Ndimile Kilatu
---
Bi Anna ameongeza kuwa, suala la kujihakikishia usafi wa mazingira kwa wote linahitaji zaidi ujengaji wa vyoo na hivyo jamii inapaswa kuhamasishwa.

“Wasichana ni moja ya kundi linaloathiriwa na ukosefu wa vyoo vya kibinafsi kutokana na mazingira yao. Vyoo bora vinamaanisha wanafunzi wanaweza kwenda shule na kupata elimu, wazazi wanaweza kulea watoto wao kwa usalama, na wanawake na wasichana wanaweza kuwa safi na salama wakati wa hedhi,” anasema.

Hali hiyo ni tofauti kwa Margaret Peter Kyaulila, msichana mlemavu wa macho, mkazi wa kata ya Azimio, Mtaa wa Mshikamano mkoani Morogoro. Yeye anasema wakati dunia ikiadhimisha siku ya choo leo, bado hali ya usafi wa mazingira ya choo anachotumia haikidhi mahitaji yake ya kila siku.

Miaka miwili iliyopita Margaret alifanya maamuzi magumu. Aliachana na wazazi wake na kuamua kuanza maisha yake binafsi ya kujitegemea.

Awali kabla hajazoea mazingira yake mapya, alishaanguka zaidi ya mara ishirini wakati akipapasa kuelekea chooni. Sasa anaishi kwa mazoea na msaada wa majirani zake ambao humwelekeza njia anapotaka kwenda haja.

“Chumba changu kipo umbali wa hatua kumi na tano au na zaidi kutokea mahala choo kilipo, kwa hiyo utaona ni kwa namna gani inaniwia vigumu kufika peke yangu, japokuwa kwa sasa nimeshazoea njia ya kupita wakati majirani zangu wanapokuwa hawapo.” Anasema Margaret ambaye kabla ya kwenda chooni inamlazimu kuchota maji kwenye kisima kilichopo uwani mwa nyumba anayoishi.

Hata hivyo, Margaret anawashukuru majirani zake kwa kumtoa kwenye zamu ya kufanya usafi wa choo wakithamini na kutambua hali aliyonayo.

Anatoa rai kwa serikali na wadau wa masuala ya usafi wa mazingira kumsaidia vifaa pamoja na choo rafiki kulingana na hali yake.

Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, Bw. Ndimile Kilatu anaamini haki sawa kwa wote linapokuja suala la usafi wa mazingira. Halikadhalika anaamini kampeni ya Nyumba Ni Choo inayoendeshwa na serikali kitaifa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itakuwa mkombozi kwa wananchi wenye changamoto ya kukosa vyoo bora.

“Kampeni hii tunaendelea nayo kwa kufanya ukaguzi na elimu ya mara kwa mara huwa inatolewa kwa kushirikiana na maofisa afya wa kata ili kuhakikisha vyoo vinakuwa visafi kwa wananchi ili kuepusha magonjwa ya mlipuko,” anasema Bw. Ndimile huku akisisitiza kuwa uhamasishaji ni moja ya kazi yao ya kila siku katika jamii.

Mtaalamu huyo wa masuala ya afya amekiri kuwa ofisi yake inatambua hali ya watu wa makundi maalumu ikiwa ni pamoja na walemavu, na wao huwa wanashauri kuwepo kwa vyoo rafiki wakati wa kukagua ramani ya ujenzi kwa maeneo yenye mkusanyiko wa watu ili kuleta usawa kwa kila mtu.

Anasema hamasa wanayoitoa kwa jamii sio tu usafi wa choo, lakini pia mtiririko mzima unaopaswa kufanywa katika kutekeleza suala hilo la usafi, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha unawaji mikono kwa kutumia maji tiririka na sabuni.

Anawashauri wananchi kuwashirikisha wataalamu wa afya pindi wanapotaka kujenga choo ili kushauri namna nzuri ya kujenga choo bora na rafiki kwa kila mtu, lengo likiwa ni kutowaacha nyuma walemavu.

Kufikia lengo la 6 la Maendeleo Endelevu ifikapo 2030 kunahitaji mbinu mpya, ustadi mkubwa na uvumbuzi.

Inabidi kuleta mabadiliko ya kudumu katika maisha ya watu. Wadau wote lazima waende sambamba na mikakati na mipango iliyokubaliwa kitaifa na kimataifa na kufanya kazi kwa njia iliyoratibiwa.

“Mipango yetu lazima iakisi ni jamii gani ya watu wako katika hatari ya kuachwa nyuma na kuweka mikakati inayohitajika kushughulikia ukosefu huo wa usawa” anasemna Mkurugnzi mkazi wa Shirika la WaterAid nchini, Bi Anna Mzinga.
Margaret Peter Kyaulila, msichana mlemavu wa macho, mkazi wa kata ya Azimio, Mtaa wa Mshikamano mkoani Morogoro.
---
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kila binadamu ana haki ya kupata huduma za usafi wa mazingira zinazotoa faragha na zinazohakikisha utu na usalama wake. Ukosefu wa usafi wa mazingira huathiri jamii nzima.

Ndio maana siku ya choo duniani kwa mwaka 2022 inaangazia athari za changamoto ya usafi wa mazingira kwenye maji ya chini ya ardhi. Inaakisi mifumo duni ya usafi wa mazingira inavyoeneza uchafu wa binadamu kwenye mito, maziwa na udongo, na kuchafua rasilimali za maji chini ya ardhi.

Inaelezwa kuwa Maji ya chini ya ardhi ndio chanzo kikubwa zaidi cha maji safi ulimwenguni. Inasaidia usambazaji wa maji ya kunywa, mifumo ya usafi wa mazingira, kilimo, viwanda na mifumo ya ikolojia. Hata hivyo, zipo taarifa za baadhi ya visima kuchimbwa katika maeneo ambayo yanaingilia na maji yatokayo kwenye vyoo.

Ni vyema watunga sera kutambua kikamilifu uhusiano kati ya usafi wa mazingira na maji ya chini ya ardhi katika mipango yao ya kulinda rasilimali hii muhimu ya maji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: