Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) imethibitisha kushindwa kutua kwa Ndege ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) yenye namba 5H-TCK katika uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera baada ya kuwepo hali mbaya ya hewa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hamza Johari imeeleza kuwa Ndege hiyo imeshindwa kutua katika uwanja huo kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa iliyohusisha mvua kubwa na kutanda kwa ukungu katika uwanja huo.

Ndege hiyo ambayo ilikuwa inaenda mjini Bukoba kupitia Mwanza ikitokea Dar es Salaam, ililazimika kutua salama katika uwanja wa Ndege wa Mwanza majira ya saa 6:56 mchana.

Ufafanuzi huo umetolewa leo baada ya mmoja wa Wabunge wa Viti Maalum, Mhe. Neema Lugangira kunukuliwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu hali hiyo ya kushindwa kutua kwa Ndege hiyo katika uwanja huo wa Ndege wa Bukoba.

“Still shaken lakini Mungu ni Mwema. Nimepanda ndege asubuhi ya leo kwenda Bukoba. Safari ilikuwa na changamoto, tumefika lakini ndege ikashindwa kutua. Nampongeza Rubani kwa uamuzi sahihi wa kurudi Mwanza na sasa narudi Dar. Serikali ibebe kwa uzito suala la airport mpya Bukoba”, ameandika Lugangira.

Aidha, Mbunge huyo wa Viti Maalum amewapongeza Rubani wa Ndege hiyo na Msaidizi wake kwa uamuzi wao sahihi wa kutua uwanja wa Ndege wa Mwanza baada ya kukumbana na hali hiyo ya hewa mjini Bukoba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: